Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC) Jaji Slivia
Fernandez de Gumendi, jana (Ijumaa), amekutana na kufanya
mazungumzo na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa
Matiafa, Balozi Tuvako Manongi
Katika Mazungumzo hayo baina ya Jaji Gumendi na Balozi Manongi
yaliyofanyika katika Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania, Rais wa ICC
aliishukuru Tanzania kwa hotuba yake iliyotolewa na Balozi siku ya
Jumatatu wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilipopokea na
kujadilia Ripoti ya ICC.
Kwa mujibu wa Rais wa ICC Jaji Slivia Fernandez de Gumendi hotuba
ya hiyo ya Tanzania ilikuwa yenye uwiano (balanced) na pia
ilitoa ushauri au mapendekezo ya namna gani Mahakama hiyo inavyoweza
kuboresha uhusiano na wanachama wake kwa mujibu wa Mkataba wa Roma.
“ Nilikusikiliza kwa makini sana wakati ulipokuwa unatoa hotuba
yako, nilinukuu kila hoja ulizokuwa unazizungumza . Hotuba ya
Tanzania ilikuwa yenye uwiano (balanced) na ningependa kuitumia
fursa hii kuishukuru Tanzania kwa hilo.
Rais huyo wa ICC amekiri kwamba anadhani ni wakati muafaka kwa wadau
wa pande mbili kukaa na kuzungumza kama ambayo Tanzania na
wanachama wengine wameshauri hasa kutokana na kile alichosema, kwamba,
kila nchi imekuwa na tafsri tofauti na uelewa tofauti kuhusu
baadhi ya vipengere (articles) zinazohusu Mkataba wa Roma unaounda
Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai.
Kwa upande wake Balozi Manongi amesema, ushauri na mapendekezo ambayo
yametolewa na Tanzania pamoja na nchi nyingine hayalengi katika
kutaka kubadili Mkataba wa Roma au kuipunguzia nguvu ya
kiutendaji Mahakama hiyo.
“Tungependa sana ieleweke kwamba tunaposhauri kukaa na kuzugumza
kusitafsiriwe kana kwamba tunataka kupunguza nguvu ya utendaji wa
chombo hiki ambacho wote tunaamini kwamba kinastahili kuwapo.
Tunashosema na kusisitiza, kwamba kila upande unahoja za msingi basi
tuzijadili kwa kuzungumza” akasisitiza Balozi Manongi.
Rais wa ICC na Balozi Manongi walibadilishana mawazo juu na masuala
mbalimbali kuhusu utendaji kazi wa Mahakama ya ICC ikiwa ni pamoja na
kuangalia ni maeneo gani ambayo Mahakama na wanachama wake wanaweza
kujadiliana .
No comments:
Post a Comment