Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar, Vuai Ali Vuai akiwahutubia Viongozi wa Halmashauri Kuu ya CCM
Mkoa wa Kusini Unguja katika Mkutano wa tathimini na majumuisho ya ziara
ya Mkoa kwenye Matawi Tisa (9) ya Chama yalipo katika Majimbo ya Mkoa
hu, pamoja na taarifa mbali mbali za utekelezaji wa shughuli mbali mbali
za kisiasa.
Na Is-haka Omar, Zanzibar.
BAADHI ya Viongozi na wanachama
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar wametakiwa kuacha tabia ya kutumia
mitandao ya kijamii kujadili masuala yanayohusu Chama badala yake
watumie vikao halali vinavyotambuliwa na Katiba ya Chama hicho.
Rai hiyo imetolewa na Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai wakati akifunga Mkutano wa
Viongozi wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kusini Unguja Kichama
uliofanyika katika Shule ya Msingi Makunduchi Mkoani humo.
Alifafanua kwamba tabia hiyo ya
kujadili, kukosoa na kuwatuhumu baadhi ya viongozi wa ngazi mbali mbali
wa Chama na Jumuiya zake kupitia Mitandao ya kijamii ni utaratibu
unaokwenda kinyume na miongozo ya chama hicho.
Alisema Katiba ya CCM inaelekeza
Kwamba mambo yote yanayogusa maslahi mapana ya Chama yajadiliwe Katika
Vikao halali vinavyotambuliwa na kanuni za Chama, kwani jukwaa hilo
ndiyo sehemu rasmi ya kukosoana na kupeana maelekezo.
Vuai alisikitishwa na tabia hiyo
na kueleza kuwa njia pekee ya kumaliza Changamoto hiyo ni Wanachama na
Viongozi kujenga utamaduni wa Kusoma na kuelewa Kanuni, Katiba na
miongozo mbali mbali ya CCM ili kufahamu wajibu, majukumu, haki na
maadili yanayoongoza Chama.
Alisema tabia hiyo imekuwa
ikifanyika katika Magroup ya Mitandao ya kijamii zikiwemo Facebook,
WhatsApp na mitandao mingine, jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa kanuni
za Chama.
“ Wanachama, Viongozi na
Watendaji naomba muelewe kwamba hiki Chama kinaendeshwa kwa utaratibu
maalum ulioelezwa Kikatiba , Kikanuni na miongozo mbali mbali, kwa nia
ya kulinda hadhi na heshima ya Chama chetu, na hakuna jambo lolote
linaloshindikana kupatiwa ufumbuzi kupitia utaratibu huo.
Sasa panapojitokeza baadhi ya
Watu miongozi mwetu wakaanza kujadili na kuwakosoa wenzao nje ya mfumo
huo basi hao tunawahesabu kuwa wana nia ya kuanzisha Majungu, Fitna na
mpasuko katika taasisi yetu.”, alieleza Vuai na Kuongeza kuwa CCM ni
Chama imara na kinachoheshimu Demokrasia katika kujadili mambo yake na
kuyatolea maamuzi stahiki katika Vikao rasmi na sio vichochoroni au
vibarazani.
Aliongeza kuwa sio kwamba kuna
viongozi na wanachama wanaogopa ama hawataki kukosolewa lakini lazima
heshima na nidhamu iwepo katika kutekeleza matakwa ya Demokrasia ndani
ya Chama hicho kwa kuheshimu utaratibu uliowekwa Kikatiba.
Akizungumzia utekelezaji wa Ilani
ya Uchaguzi ya Chama hicho ya mwaka 2015/ 2020 katika Mkoa huo
aliwapongeza Viongozi wa Majimbo wakiwemo wabunge, wawakilishi na
Madiwani huku akiwasisitiza Viongozi wa Chama kuhakikisha wanakagua
kikamilifu miradi inayotekelezwa na viongozi hao ili kujiridhisha kama
inawanufaisha wananchi wote.
Aliwataka viongozi wa Chama na
Jumuiya zake kuwa wa kwanza kutambua kero na changamoto za wananchi wa
maeneo mbali mbali na waziwasilishe kwa Wakuu wa Wilaya (DC) ili ziweze
kupatiwa ufumbuzi wa kudumu na Serikali.
“ Huu sio wakati wa kusubiri
taarifa zinazohusu Changamoto za Chama, Jumuiya na Serikali ziletwe
Ofisini, badala yake mtoke na kuzitafuta wenyewe ili kuwasaidia
wanachama na wananchi kutatuliwa kero zao kwa haraka kupitia Mamlaka
husika.”, alisisitiza Vuai.
Alisema Viongozi wanatakiwa
kufahamu kwamba suala la kuwatumikia wananchi sio jambo la hiari bali ni
lazima watekeleze kwa vitendo ahadi walizotoa wakati wa kampeni kwani
wasipotekeleza Wajibu wao vizuri kwa jamii mwisho wa siku kitakacho
hukumiwa ni Chama na sio kiongozi husika.
Aidha aliwakumbusha viongozi hao
kwamba Chama na Jumuiya zake wanatarajia kufanya Uchaguzi mwaka 2017,
hivyo waanze mapema kuwaelimisha, kuhamasisha na kuwaandaa kisaikolojia
wanachama wa Chama hicho juu ya matumizi sahihi ya kanuni za UChaguzi
ili kuepuka lawama zisizokuwa za lazima.
Alisema Wanachama wanatakiwa
kuwachagua viongozi wenye sifa na wasiokuwa na Mukhari( kuoneana haya)
katika kusimamia mambo ya msingi ya CCM na waumini wa kweli wa
Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Muungano wa Serikali mbili wenye
vigezo hivyo ndio wanaofaa kuwa viongozi.
Hata hivyo aliwapongeza Rais wa
Zanzibar, Dkt. Shein na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Magufuli kwa juhudi na kasi zao za kufanikisha mipango ya maendeleo ya
nchi kwa ufanisi mkubwa hali inayoongeza hamasa kwa jamii kuendelea
kuwaamini.
Mapema Katibu wa CCM Mkoa huo,
Sauda Mpambalyoto akiwasilisha taarifa ya tathimini ya ziara ya wajumbe
wa Kamati ya siasa ya Mkoa na Jumuiya za CCM, alisema lengo la ziara
hiyo ni kukutana na wanachama na viongozi walioko ngazi za mashina,
matawi ambao wao ndio wanaozijua kero za wananchi ili zitafutiwe
ufumbuzi kwa wakati.
Katibu huyo akizungumzia hali ya
kisiasa alisema inaendelea kuimarika kutokana na asili ya Mkoa huo kuwa
ndio ngome ya CCM, licha ya kuwepo na makundi yaliyopandikizwa na
wapinzani kwa nia ya kuharibu Umoja na Mshikamano wa wanachama wa Chama
hicho.
Alisema baadhi ya maeneo ya Mkoa
huo wanakabiliwa na Changamoto ya upungufu wa Maji Safi na salama
kutokana na Ongezeko la Idadi ya Watu na Uchakavu wa mioundo mbinu.
Alizitaja changamoto zingine kuwa
ni pamoja na ukosefu wa huduma za Afya kwa baadhi ya maeneo
zinazotokana na upungufu wa Madaktari.
Kupitia Mkutano huo aliwapongeza
Wanachama wote wa Mkoa huo kwa kushirikiana vizuri na viongozi na
watendaji wa Chama na Serikali na kuwasihi watendaji wenzake, kufanyia
kazi kwa Vitendo nasaha na maelekezo yaliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu
wa CCM Zanzibar, ili kujenga Chama kitakachokuwa na faida kwa vizazi vya
sasa na vijavyo.
No comments:
Post a Comment