Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Serikali kupitia Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia imewapangia vyuo wanafunzi wa programu maalum ya
ualimu chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) ambao hawakupata nafasi ya vyuo
katika awamu ya kwanza, walioagizwa kuomba mafunzo kulingana na sifa zao
kupitia Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi (NACTE).
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo leo, jijini Dar es Salaam
alipokuwa akitoa taarifa kuhusu wanafunzi wanaosoma stashahada maalum ya
ualimu wa sayansi chuo kikuu cha Dodoma.
“Mtakumbuka tuliagiza kwamba
wanafunzi ambao walikosa sifa za kujiunga na ualimu wa sayansi waliombwa
kuomba mafunzo yanayolingana na ufaulu wao kupitia NACTE, Lakini baada
ya taarifa hiyo tulipokea maombi mengi kutoka kwa vijana hawa wakiomba
kupangiwa vyuo moja kwa moja na Wizara, wizara imetafakari na kuamua nao
wapangiwe vyuo vya Serikali,” alifafanua Dkt. Akwilapo.
Aliendelea kusema kuwa, wanafunzi
ambao waliachwa awamu ya kwanza na kupangiwa katika awamu ya pili ni
wanafunzi 290 ambao walikuwa wakisomea programu ya stashahada ya ualimu
wa sekondari na wanafunzi 1,181 ambao walikuwa wakisomea stashahada ya
ualimu wa msingi.
Dkt. Akwilapo amesema kuwa Wizara
imeamua kuwapangia wanafunzi hao vyuo kutokana na kuonyesha nia ya dhati
ya kusomea ualimu ambapo wanafunzi hao wamepangiwa vyuo vya ualimu vya
Marangu na Tabora.
Aidha, Dkt. Akwilapo ameeleza kuwa
wanafunzi hao watajigharamia masomo yao kulingana na viwango vya ada
vilivyowekwa na Serikali. Pia amewataka kutembelea tovuti ya wizara ya
hiyo ambayo ni www.moe.go.tz ili kuona vyuo walivyopangiwa.
Mnamo tarehe Mei 28, 2016 Serikali
iliwarejesha nyumbani wanafunzi 7,805 waliokuwa wanasoma Stashahada
Maalum ya Ualimu wa Sayansi na Hisabati katika Chuo Kikuu cha Dodoma.
Katika mchujo wa awamu ya kwanza wanafunzi 382 ndio waliokuwa na sifa ya
kuendelea na masomo chuo kikuu cha UDOM na wengine 4,586 walipangiwa
vyuo vya ualimu vya Serikali.
No comments:
Post a Comment