Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara, Bibi. Janeth Mayanja akiwa ofisini kwake.
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara, Bibi. Janeth Mayanja
amemsimamisha kazi mtumishi wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji kwa kosa
la kujipatia fedha kinyume na taratibu za utumishi wa umma.
Akizungumza leo mjini Bunda wakati
wa tukio hilo, Bibi. Mayanja alisema kuwa ameamua kumsimamisha kazi
kwa muda, Bw.Eliudi Haonga ambaye ni mtumishi wa Idara ya Ardhi na
Mipango Miji pia ni Mthamini wa Halmashauri hiyo ili kupisha uchunguzi
kwa kosa la kujipatia fedha kinyume na taratibu za utumishi wa umma.
“Tarehe 28 mwezi Juni mwaka huu
Bw.Eliudi Haonga alipokea fedha kiasi cha shilingi milioni saba
kutoka kiwanda cha Olam ikiwa ni kodi ya pango kwa mwaka kodi
2015/2016, lakini mtumishi huyo alihifadhi kwenye akaunti ya
Halmashauri ya mji yaani ‘own source’ fedha kiasi cha shilingi milioni
mbili tu, na kiasi kilichobaki yaani milioni tano alizitumia kwa
masuala binafsi kinyume na taratibu za utumishi wa umma” alisema Bibi
Mayanja
Aliongeza kuwa Bw. Haonga aligushi
risiti ya Halmashauri ya Mji na ambayo aliikabidhi katika kiwanda cha
Olam baada ya kupokea fedha hizo.
Alisisitiza kuwa mtumishi huyo
amesimamishwa kazi kwa mujibu wa kifungu namba 38 (1) cha kanuni za
utumishi wa umma za mwaka 2003.
Aidha, Bibi Mayanja amewaasa
watumishi wa umma wanaofanyakazi katika Halmashauri hiyo kuwa
waadilifu kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi. Vile vile
ameonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote
atakayekiuka.
No comments:
Post a Comment