Msemaji wa CCM, Christopher Ole
Sendeka akizungumzaa Waandishi wa Habari, kufafanua masuala mbalimbali,
katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba Jijini Dar es Salaam.Ifuatayo ni Taarifa rasmi Kama ilivyosomwa na Sendeka wakati wa kikao hicho na waandishi wa Habari.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu wanahabari,
Chama cha Mapinduzi (CCM)
kimepokea kwa majonzi na masikitiko makubwa sana taarifa ya kushambuliwa
na kuuawa kwa askari wa jeshi la Polisi wakiwa katika kutekeleza
majukumu yao ya ulinzi eneo la Mbande, Temeke jijini Dar Es Salaam.
CCM tayari imemtumia salamu za
rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Ernest Mangu pamoja na familia za
marehemu waliofikwa na umauti katika tukio hilo baya katika historia ya
nchi yetu.
Tunalaani tukio hilo na kutoa wito
kwa wananchi kuvipa ushirikiano wa kutosha vyombo vya dola ili
kufanikisha wahusika wa tukio hilo kusakwa popote pale na kupatikana ili
wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria haraka.
Serikali ya Chama Cha Mapinduzi
itaendelea kuhakikisha amani ya Taifa letu inalindwa dhidi ya wachache
wanaofurahia madhila kwa wananchi wetu. Wananchi wetu wanapenda,
wamezoea na wanastahili amani. Ndio maana Tanzania imekuwa nchi ya
kupigiwa mfano, ikionesha uongozi katika maeneo mengi. Tuendelee
kuilinda taswira hii.
MAFANIKIO YA AWAMU YA TANO
Ndugu wanahabari,
CCM inachukua nafasi hii
kumpongeza Rais Mhe Dkt John Pombe Magufuli na Serikali yake kwa
mafanikio makubwa yaliyopatikana katika muda mfupi wa uongozi wake.
Rais Magufuli aliahidi mabadiliko.
Tunampongeza kwa kusimamia vema utekelezaji wa ilani ya CCM. Katika
muda mfupi wa miezi tisa tu, Rais Dk Magufuli amefanya mambo makubwa.
Sote tunafahamu kuwa Shirika letu
la Ndege, ATCL, limekuwa linafanya kazi na ndege moja. Serikali ya Dk
Magufuli imekwisha lipia ndege tatu za abiria toka Canada, ndege mbili
zitaingiza nchini mwezi ujao.
Reli ya kati inajengwa kwa kiwango
cha Standard Gauge. Meli katika ziwa viktoria inanunuliwa ktk bajeti ya
mwaka huu. Elimu ya msingi na sekondari inatolewa bure. Wanafunzi wetu
sasa wanakalia madawati na kujifunza vizuri zaidi. Barabara zimeendelea
kujengwa. Makusanyo ya kodi yameongezeka. Huduma za jamii zinaendelea
kuimarika. Lakini pia, nidhamu katika utumishi wa umma sasa imeimarika.
Wananchi wanastahili huduma nzuri na kuthaminiwa na wafanyakazi wa Umma.
Mataifa mengi ya Afrika na nje ya
Afrika yanaiga mbinu za Rais wetu katika kuleta mabadiliko nchini mwao.
Hapa Kenya tu, Waziri mmoja wa Elimu anayesifika kwa utendaji kazi
mzuri, anajiita “MAGUFULI.” Hata Australia, baadhi ya wananchi waliwahi
kumtaka Waziri Mkuu wao afanye kazi kama Dk Magufuli.
Dk. Magufuli ameazimia kujenga
uchumi wa viwanda. Ifikapo mwaka 2025, Tanzania itakuwa nchi yenye
uchumi wa kati. Maisha ya wananchi wetu yataboreka. Vijana wetu wapate
ajira katika viwanda, watauza malighali na mahitaji mbalimbali ya
viwanda. Wakulima watapata masoko ya bidhaa zao katika viwanda hivyo.
Kilimo kitaongezeka thamani kutokana na mahitaji mbalimbali ya viwanda
vyetu. Hatua za kuelekea huko tayari zimechukuliwa.
Wapo wachache wanaelekea kutafuta
mbinu chafu za kuhujumu mafanikio haya, lakini hawatafanikiwa.
Watanzania wamemchagua Dk Magufuli ili awaletee maendeleo.
Serikali ya CCM, itawasaidia
vijana wa Tanzania kuendesha uongozi wa Taifa lao. Kamwe tusikubali
ndoto ya kuongoza mapinduzi haya makubwa kwa ajili ya Taifa na Bara letu
ikapokonywa na watu wachache wasiokuwa na dira ya kuliletea maendeleo
Taifa letu. Tuwapuuze.
UPINZANI KUSUSIA VIKAO VYA BUNGE
Ndugu Wanahabari,
Bunge kama ilivyo kwa mhimili
mingine linaongozwa kwa katiba, sheria na kanuni katika mijadala na
maamuzi yake. Kama Mbunge hajaridhika na maamuzi ya Spika, Naibu Spika
au Mwenyeki wa kikao, kuna taratibu za kufuata. Utaratibu wa kikanuni ni
kuulalamikia uamuzi huo kwa Katibu wa Bunge. Wakiwa wanafahamu taratibu
za kikanuni, kama kawaida yao, WAPINZANI, waliamua kuzisigina na badala
yake wakataka Naibu Spika aondolewe.
Hivyo wakaratibu kupigwa kura ya
kutokuwa na imani na Naibu Spika. Ambapo suala hilo lilipelekwa kwenye
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Kutokana na kutokuwepo kwa
Spika nchini, hoja hiyo haikufikia ukomo. Tunamshukuru Mungu afya ya
Spika imeimarika. Sasa hoja hiyo huenda itafikishwa katika mkutano wa
Bunge litakalokaa mwezi ujao.
Kana kwamba hiyo haitoshi, kama
kawaida yao, hawakuwa na subira ya kufuata taratibu. Wakaamua kufanya
kihoja. Wakaamua kutohudhuria vikao vyote vya Bunge vilivyokuwa
vikiongozwa na Naibu Spika.
Na hata walipoingia Bungeni
waliziba midomo yao na kuamua kutowasalimia wabunge wenzao wa CCM,
kutopeana mikono na hata kutohudhuria misiba na sherehe zao. Vitendo
vyao hivi ndivyo vimeasisi chuki ndani ya jamii yetu iliyozoea UPENDO,
UDUGU, UMOJA NA MSHIKAMANO. Watanzania tunafahamika na tunaona fahari
kuishi kama ndugu.
Baada ya kitendo hicho cha
kuwasaliti wapigakura wao kulaaniwa kila kona ya nchi, sasa wamekubali
kutumiwa kama vibaraka kuichafua taswira ya nchi yetu, nao kwa hila
iliyo wazi, wamekubali kuwafitinisha watanzania kwa kuandaa maandamano
ya nchi nzima, yasiyo na ukomo. Hatua hii ni uvunjaji wa katiba ya nchi,
Sheria na inalenga kuvunja amani, utulivu na mshikamano wa watu wetu.
Ileleweke kwamba, wanachokifanya
hawa CHADEMA ni kuchochea wananchi kwa makusudi kutotii maagizo halali
ya vyombo vya dola na Serikali kwa visingizio mufilisi kuwa katika
Katiba imewapa uhuru huo. Katika haitoi haki na uhuru usio na ukomo.
Ibara ya 29 (5) inasema;
“Ila watu wote waweze
kufaidi haki na uhuru vinavyotajwa na katiba hii kila mtu ana wajibu wa
kutenda na kuendesha shughuli zake kwa namna ambayo haitaingilia haki na
uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma”
Baada ya kusema hayo, ninaomba
CHADEMA wakumbuke na kutilia maanani kuwa kila haki ina wajibu na hakuna
haki au uhuru usiokuwa na ukomo hususani pale inaposababisha kuingiliwa
ama kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine. Rejea ibara ya 30 (1)
na (2) ya Katiba.
Ndugu wahabahari,
Mwisho tunatoa pole kwa wenzetu wa
CUF kutokana na mapambano huko kwao. Tumestushwa sana na yanayoendelea
huko. CCM inawapa pole na tunawatakia maelewano ili waje tusaidiane
kuwaletea watanzania maendeleo.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI.
No comments:
Post a Comment