Friday, 26 August 2016

Wabunge Simba: Mo apewe timu

 Bilionea Mohamed Dewji ‘Mo’.

Katika kile kinachoakisi mapinduzi ya kweli kwenye soka la Tanzania, nao wabunge wanachama na wapenzi wa Simba wameridhia kwa kauli moja azimio la mpango wa uongozi wa klabu hiyo kumuuzia timu, bilionea Mohamed Dewji ‘Mo’.
Kauli ya wabunge imekuja kipindi muafaka baada ya wanachama kuridhia mpango huo ambao Mo ameshaweka bayana kuwekeza kitita cha Sh bilioni 20 kwa kununua hisa za asiliamia 51 huku Simba ikivuna kitita cha Sh bilioni 3.5 kwa mwaka.

 Mwenyekiti wa Simba- Wabunge, Juma Nkamia.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Simba- Wabunge, Juma Nkamia ambaye amesema kwa kauli moja wabunge wanachama wa klabu hiyo wameridhika Mo kuuziwa hisa hizo baada ya kulitafakari kwa mapana yake na kuona uwekezaji wake una tija kubwa katika maendeleo ya Simba.

Kikosi cha timu ya Simba.

“Sisi kama wabunge tunaunga mkono mpango wa Mo kwani una lengo la kuifanya Simba kuwa moja ya klabu bora kabisa barani Afrika, kwa sababu wanachama watakuwa huru kununua hisa ambao watakuwa na mamlaka ya kuendesha klabu hiyo katika mfumo huu,” alisema Nkamia na kutolea mfano uwekezaji ulivyozibadili klabu mbalimbali za Ulaya ambazo awali zilikuwa ni miliki ya wanachama lakini leo hii ni tishio duniani, si uwanjani tu bali kiuchumi.

“Arsenal, Manchester United, Real Madrid zote zilikuwa na mfumo wa kumilikiwa na wanachama, kadiri ya muda zimekuja na mabadiliko ya mfumo wa muundo huu wa kuwekeza ambao umezifanya kuwa klabu kubwa duniani. Tunaamini kwa uwekezaji wa Mo Simba itaweza kushindana na klabu kubwa barani Afrika kama TP Mazembe (DR Congo) na Al Ahly ya Misri,” aliongeza Nkamia.

No comments:

Post a Comment