Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (Mb) (kulia) akimkabidhi cheti Mwanariadha
Alphonce Simbu baada ya kuibuka mshindi wa nafasi ya tano katika
Mashindano ya Olimpiki yaliyomalizika hivi karibuni mjini Rio, Brazil.
Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (Mb) (kulia) akimkabidhi
King’amuzi cha Kampuni ya DSTV Mwanariadha Alphonce Simbu baada ya
kuibuka mshindi wa nafasi ya tano katika Mashindano ya Olimpiki
yaliyomalizika hivi karibuni mjini Rio, Brazil.
Rais wa Shirikisho la
Riadha Tanzania (RT) Bw. Anthony Mtaka akiongea na baadhi ya Viongozi,
wageni waalikwa pamoja na Wanamichezo (hawapo pichani) walioshiriki
katika Mashindano ya Michezo ya Olimpiki yaliyomalizika hivi karibuni
mjini Rio, Brazil.
Mwenyekiti wa Kamati
ya Olimpiki (TOC) Bw. Filbert Bayi akiongea na baadhi ya Viongozi,
wageni waalikwa pamoja na Wanamichezo (hawapo pichani) walioshiriki
katika Mashindano ya Michezo ya Olimpiki yaliyomalizika hivi karibuni
mjini Rio, Brazil.
PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM.
Na Benedict Liwenga-WHUSM.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape
Nnauye amewataka Watanzania kujifunza kuwatia moyo Wanamichezo
wanaposhiriki katika michezo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Wito huo ameutoa jana Jijini Dar es Salaam wakati wa Hafla
ya kuwapongeza na kupokea bendera ya Taifa toka kwa Wanamichezo ambao
walishiriki katika Mashindano ya Olimpiki yaliyomalizika hivi karibuni
mjini Rio, nchini Brazil.
Mhe. Nnauye alisema kwamba, Watanzania ni vizuri
wakajifunza kusema maneno mazuri kwa wanamichezo pindi wanaporejea toka
katika Mashindano mbalimbali ili kuwapa moyo wa kuendelea kufanya vizuri
wanamichezo hao huku akisisitiza kuwa, ni vema ukosoaji ukaendana na
ushauri mzuri wenye kujenga badala ya kulaumu.
Aliongeza kuwa, Wanahabari nchini wanapaswa kuandika
mazuri yanayofanywa na wanamichezo kwani yana manufaa kwa Taifa badala
ya kutafuta maneno yasiyo na tija ya kukosoa mara kwa mara kwani kuna
wavunja moyo wanamichezo.
“Tukijifunza kuandika na kusema mabaya tu ya kuvunja moyo
kwa wanamichezo wetu hii sio sawa sawa, tujifunze kuwatia moyo, na hii
ni hatua ya kwanza na wito wangu kwa Watanzania wote”, alisema Mhe.
Nnauye
Alisisitiza kwamba, Watanzania wanapaswa kujifunza
kujivunia vitu vya kwao kwa njia hiyo itakuwa ikiongeza hamasa kwa
wanamichezo katika kujituma kwa manufaa yao na ya Taifa.
Aidha, alisisitiza kuwepo na maandalizi ya mapema kwa
Wanamichezo nchini ili waweze kufanya vizuri zaidi huku akishauri
uwekezaji wa kutosha katika sekta hiyo na kuyataka Makampuni kuwa na
tabia ya kuwatumia Wanamichezo nchini katika kutangaza utalii wa nchi.
Ametoa wito kwa Viongozi wazembe ambao watashindwa kufikia
malengo mazuri katika tasnia hiyo ni bora wakaachia ngazi zao ili kuwapa
nafasi watu wengine wenye uwezo kutekeleza kazi hiyo.
“Nadhani sasa tuanze kukabana kwenye Vyama, ukichaguliwa na
kukawa na mashindano kama haya, ukashindwa kupeleka hata mchezaji
mmoja, kazi yako ya kwanza nadhani ni kijiuzulu”, alisema Mhe. Nnauye.
Awali akitoa taarifa ya Wanamichezo walioshiriki katika
Mashindano hayo, Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Bw. Gulam
Rashid alisema kwamba, Tanzania ilishiriki mashindano hayo ikiwa na
Wanamichezo saba, walimu wa tatu wa michezO ya kuogelea, Judo na riadha
ambapo kati yao wachezaji wa nne walipata nafasi ya upendeleo (Universality).
Alifafanua kuwa, wachezaji wa nne waliofanikiwa kupata
nafasi ya upendeleo ni wale ambao walishiriki katika michezo mbalimbali
katika kusaka viwango, lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kufikia
viwango vinavyowaruhusu wao kushiriki katika mashindano hayo, hivyo
kulingana na Sera na itikadi za Olimpiki zilitaka kila nchi Duniani
ambayo ni Mwanachama wa Mashindano hayo kutoa watu wake, hivyo walitoa
nafasi hiyo kwa wale waliokosa kufikia viwango kuweza kushiriki.
“Nchi ambayo haikuwa na wachezaji waliofikia viwango vya
Olimpiki walipewa nafasi ya upendeleo kwa wanamichezo kuweza kushiriki
na kwa Tanzania tulikuwa na Waogeleaji wa tatu, mchezaji wa Judo na
mchezaji wa kike wa mbio (Marathon) kwa hiyo, huo ndiyo upendeleo ambao
wengi hawauelewi ni upendeleo upi”, alisema Bw. Gulam.
Aidha, katika hafla hiyo, mbali na kukabidhiwa Bendera ya
Taifa toka kwa kikosi hicho cha Wanamichezo walioshiriki katika Olimpiki
2016mjini Rio-Brazil, Mhe. Nnauye kwa niaba ya Makampuni ya TTCL na
DSTV-Multi Choice aliwapatia zawadi mbalimbali washiriki hao zikiwemo
fedha taslimu ambapo kwa nafasi ya kipekee Mwanariadha Alphonce Simbu
ambaye aliibuka katika nafasi ya tano katika Mashindano hayo amepatiwa
Mkataba wa mwaka mmoja wa kuwa Balozi wa DSTV ambapo kila mwezi atakuwa
akilipwa kiasi cha Shilingi milioni moja pamoja na king’amuzi maalum,
huku washiriki wengine wakipewa ving’amuzi na fedha.
No comments:
Post a Comment