Wednesday, 31 August 2016

Mbarali kwafurika watu wa kushuhudia kupatwa kwa jua

Mbarali. Maelfu ya watu kutoka  ndani na nje ya nchi  wakiwemo wasomi na wanafunzi wametua katika mji mdogo wa Rujewa wilayani hapa, kwa lengo la  kushuhudia tukio la kihistoria la kupatwa kwa jua kuanzia saa 4.15 asubuhi hadi saa 7.59 mchana kesho Septemba Mosi.
Tukio hilo  la kihistoria  limevuta  umati wa watu na kusababisha msongamano mkubwa kwenye mji na viunga vyake.
Aidha tukio hilo limesababisha nyumba zote za wageni katika mji huo kujaa huku watu wakiendelea kumiminika na wengi wakionekana kukosa sehemu za malazi na kuamua kurudi jijini Mbeya.

Akizungumzia tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Mbarali  ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, Reuben Mfune alisema hali ya ulinzi na usalama katika wilaya hiyo ipo vizuri na kuwahakikishia wananchi wote na wageni waliofika kutokuwa na hofu yoyote licha ya kuwapo kwa changamoto ya kukosa malazi.

Mfune alivipongeza vyombo vya habari takribani vyote kutua kwenye wilaya hiyo na kufanya kazi kubwa ya kuwahamasisha wananchi jambo ambalo litasaidia zaidi kuitangaza wilaya hiyo yenye vivutio vingi vya utalii.

No comments:

Post a Comment