Wagombezi wakuu ni rais aliye
maamlakani Ali Bongo, na mpinzani wake mkuu, Jean Ping, ambaye alikuwa
kiongozi wa zamani wa tume ya umoja wa Afrika.
Rais Bongo alichukua wadhfa wa urais mwaka 2009 baada ya kifo cha babke Omar Bongo.
Rais Bongo ana nafasi kubwa ya
kushinda uchaguzi huo, kwani anadhibiti serikali, na mshindi anahitaji
kumzidi mpinzani wake kwa kura moja pekee.
Hata hivyo upinzani umelezea wasiwasi kwamba serikali tayari ‘imetayarisha matokeo’
Bwana Ping ana uhusiano wa karibu
na familia ya Bongo, kwani kwa wakati mmoja alikuwa shemejiye rais Ali
Bongo, baada ya kumwoa dadake.
Ijumaa, katibu mkuu wa umoja wa
mataifa Ban Ki-moon alitoa wito kwa pande zote mbili kudumisha amani,
kabla na baada ya uchaguzi.
Wagombea kumi wanawania wadhfa wa urais.
Bwana Ping, 73, ameungwa mkono na
vigogo wawili wa upinzani ambao pia walikuwa washirika wa karibu wa
familia ya Bongo: Casimir Oye Mba, waziri mkuu wa zamani na aliyekuwa
spika wa bunge Guy Nzouba Ndama.
Katika kampeni za uchaguzi huo,
chama cha rais Ali Bongo Gabonese Democratic Party (GDP) kimekuwa
kikiwapa watu zawadi, zikiwemo simu, jokofu na mashine za kufua nguo.
Mshindi wa uchaguzi huo, ataongoza kwa muhula wa miaka saba.
Gabon ni miongoni mwa wazalishaji wakuu wa mafuta barani Afrika, japo theluthi ya raia wake ni maskini.
Raia wa Gabon ni milioni 1.5 pekee.
No comments:
Post a Comment