Muonekano wa jua litakavyokuwa wakati wa kupatwa kwa jua.
Tukio hilo linatazamiwa kuanzia saa 4:17 asubuhi hadi 7:56 adhuhuri siku hiyo.
Mashabiki na wanataaluma wa anga kutoka duniani kote pamoja na wanasayansi, wanafunzi pamoja na jamii ya Tanzania wataelekea Rujewa, kusini mwa Tanzania, karibu na Mbeya, kushuhudia duara la Jua linavyobadilika kuwa mithili ya pete.
Watu wanaoishi ndani ya ukanda wenye upana wa kilometa 100 unaokatisha kusini mwa Tanzania, kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuelekea Katavi, Mbeya, Ruvuma hadi Masasi na kuingia Msumbiji, siku hiyo wataona jua kama duara jembamba mithili ya pete, kwa vile asilimia 98 ya jua katika maeneo yao litakuwa limejificha nyuma ya mwezi. Kupatwa huko kwa jua kunaweza kuonekana kwa usalama na watazamaji, lakini inabidi kutumia vichuja maalum vya mwanga wa jua.
Tukio la kupatwa kwa jua ni la kusisimua na la nadra sana kutokea katika maisha ya mtu na baadhi ya dini kama Uislamu zinawataka watu wakati wa kipindi hicho kuwa kwenye swala maalumu. Vijana wengi katika kizazi hiki kipya watakuwa hawajaona tukio hili na hivyo ni tukio litakalowasisimua na wanafunzi ambao wamekuwa wakijifunza mashuleni watapata ushahidi wa moja kwa moia siku hiyo.
Kupatwa huku kwa jua kutatokea siku ya Alhamisi ambapo wanafunzi wengi watakuwa shuleni na litatokea wakati wa masomo. Kwa vile mchakato wote utaendelea kwa masaa manne hivi, kati ya saa 4:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana wanafunzi wataweza kushirikiana kuangalia, kusimulia na kujadili tukio ili kulielewa vizuri na kuandika ripoti madarasani mwao. Tukio jingine kubwa la kupatwa kwa Jua kama hili halitatokea miaka 15 ijayo, kwa hiyo tunahitaji kutumia fursa hii kwa ukamilifu kujifunza.
Ili kuangalia kupatwa huko, kila mmoja atahitaji kutumia kikinga macho kinachochuja mwanga wa Jua kiitwacho Kitazamia Jua. Nini hatari kuangalia jua lililopatwa kwa macho moja kwa moja au hata kutumia vichujio vingine vya kiza vilivyotengenezwa mitaani. Kitazamia Jua maalumu ni kifaa rahisi kilichotengenezwa kutokana na kichuja nguvu ya jua ambacho kinaondoa mionzi haribifu kwa asilimia 99.999.
Miwani hiyo maalumu ya Jua inaweza kutengenezwa Tanzania kwa gharama isiyozidi Sh 500 kila moja, ikiwemo kuchapa fremu za kadbodi na kichuja nguvu ya jua (polymer filter) kinachoagizwa kutoka Marekani.
No comments:
Post a Comment