Rais Robert Mugabe amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri ambalo
amewaondoa baadhi na kuingiza sura mpya lakini habari kubwa ni kushushwa
kwa makamu wa rais wake, Emerson Mangagwa.
Katika mabadiliko hayo, Mangagwa sasa atakuwa waziri wa utalii hali ambayo imetafsiriwa kwamba ameshushwa cheo.
Shirika la habari la ZimNews, likinukuu chanzo cha uhakika kutoka ndani
ya serikali limesema Mnangagwa alikwishadokezwa kujiandaa kwa makubwa
yanayotarajia kumfika na sasa amepokonywa nafasi zote za makamu wa rais
na ile ya makamu wa rais katika chama tawala cha Zanu-PF.
Wakati fulani Mnangagwa alikuwa anapewa nafasi ya kumrithi Mugabe ikiwa
atafariki dunia au kuamua kung’atuka. Lakini katika siku za hivi
karibuni alianza kutopikika na wenzake hususan mke wa Raus Mugabe, Grace
Mugabe.
Mnangagwa aliwahi kushutumiwa na mwanamama huyo kwamba anashirikiana na
watu waliofukuzwa Zanu PF. Pia, alishutumiwa na Grace kuwa alikuwa
anafanya njama za kutaka kumpindua rais ili arithi nafasi yake.
Kilichomponza zaidi ni king’ang’anizi chake kwamba alikula sumu
iliyokuwemo kwenye Ice Cream kutoka kampuni ya maziwa inayomilikiwa na
Grace na akapelekwa Afrika Kusini kwa matibabu. Rais Mugabe alisema
aliambiwa na madaktari waliokuwa wanamtibu makamu huyo wa rais kwamba
kuugua kwake hakukutokana na sumu, lakini yeye alishikilia kwamba
alilishwa sumu hali iliyoonekana ni kumdhalilisha Rais Mugabe.
Haya yakiwa hivyo, ndani ya Zanu PF kuna makundi makubwa mawili
yanayonyukana kuwania uteuzi wa kugombea urais; la kwanza linaitwa G40
ambalo kuna makamu wa Rais Phelekezela Mphoko huku likiungwa mkono na
Grace, na la pili linaitwa Lacoste ambalo linaongozwa na Mnangagwa. Kwa
mabadiliko haya ni kama makamu huyo wa rais amepunguzwa kasi.
Aliyekuwa Waziri wa Fedha Patrick Chinamasa nafasi yake imechukuliwa na
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Ignatius Chombo, ambaye ni katibu
mkuu wa Zanu PF anayehusika na masuala ya utawala. Wadadisi wa masuala
ya siasa wameshtushwa na uteuzi huo wakihoji atafanya nini kuhusu sarafu
ya Zimbabwe ambayo inaendelea kushuka.
Chinamasa amepewa wizara mpya isiyofahamika ya Usalama wa Mitandao. Muda
mfupi baada ya kupewa nafasi hiyo, mwigizaji maarufu Carl Joshua Ncube
alitania: "Jamani Patrick Chinamasa anawafuatilia kwenye Twitter ".
Aliyekuwa Waziri wa Utalii, Walter Mzembi sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.
Mpwa wa Mugabe, Patrick Zhuwao anayeonekana kuwa mfuasi mkuu wa kundi la
G40 linalopigiwa upatu na Grace ameteuliwa kuwa Waziri wa Kazi akitokea
Wizara ya Vijana na Utamaduni.
Hatua ya kupandikwa kwake ni ushahidi wa kutosha kwamba umelenga kulipa
nguvu kundi la G40 dhidi ya lile la Mnangagwa linaloitwa Lacoste.
No comments:
Post a Comment