Papa, ambaye pia ametoa wito wa amani duniani, amewataka waumini wote kuungana naye katika sala kwa lengo hilo maalamu na hasa kwa Kenya ambako mvutano uko juu katika mkesha wa uchaguzi wa marudio wa rais wenye ushindani mkubwa uliopangwa kufanyika Oktoba 26.
“Nawaomba wote kuungana nami katika sala ya kuombea amani ya dunia,” alisema Papa alipowaambia mahujaji na watalii waliokuwa wamekusanyika kwa ibada Jumapili.
“Nafuatilia kwa karibu sana siku hizi hali ya Kenya, ambayo niliitembelea mwaka 2015, na ambayo ninaiombea, kwamba nchi nzima iweze kukabiliana na hali ngumu ya sasa katika mazingira ya majadiliano ya kujenga, wakiwa na lengo mioyoni ya kutafuta mema.”
Mgogoro nchini Kenya umefkia hali ya mkwamo tangu Mahakama ya Juu ilipofuta matokeo ya urais ya uchaguzi wa Agosti 8 ikitaja “dosari” na “ukiukwaji” wa mchakato wa uchaguzi.
Katika uchaguzi huo zaidi ya watu milioni 15 walishiriki na matokeo yalipotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Rais Uhuru Kenyatta alipata asilimia 54 huku mpinzani wake mkuu Raila Odinga akipata asilimia 44.
IEBC imeandaa uchaguzi wa marudio Oktoba 26 kama ilivyoamriwa na Mahakama ya Juu lakini Odinga amejitoa, akisema hatashiriki hadi yafanyike marekebisho makubwa katika Tume hiyo ikiwemo kuondolewa kwa sekretarieti iliyokuwa inaongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Ezra Chiloba.
Katika kusisitiza msimamo wake Odinga ameitisha maandamano makubwa ya wafuasi wake nchi nzima Jumanne na Jumatano yakiwa na lengo la kuhakikisha uchaguzi haufanyiki kama ilivyopangwa.
No comments:
Post a Comment