Wednesday 18 October 2017

Dkt. Kigwangalla atembelea meli ya Mfalme wa Oman

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Dkt.Hamisi Kigwangalla amesema  Tanzania na Nchi ya Oman wamefanya mazungumzo ya pamoja ya namna ya kukuza sekta ya Utalii baina ya nchi hizo mbili ambapo watashirikiana katika muingiliano wa Watalii watakaokuwa wakitokea moja kwa moja Oman na kuja Tanzania.
“Tumeweza kuzungumzia ushirikiano wa sekta ya Utalii. Hii ni pamoja na kuanzisha soko la pamoja  kati ya Oman na Tanzania. Watalii wanaokwenda Oman wanaotaka kuja nchi za Afrika basi waunganishwe moja kwa moja kutoka Oman na kuja Tanzania kwani wenzetu wana watalii wengi kuliko sisi. Hivyo ujio wao hapa nchini ni faida kubwa kabisa na tumejifunza mengi katika sekta hii.
"Pia tumeweza kujifunza namna wenzetu wanavyoitangaza nchi yao  na sisi tutatumia uzoefu huo kuboresha sekta hii ya Utalii kama dhamana tuliyopewa” alieleza Dk. Kigwangalla.
Awali Dk. Kigwangalla aliweza kutembelea meli hiyo ya kifahari ya Mfalme wa Oman Mhe. Qaboos bin Said ‘Fulk Al Salamah’ iliyofika mapema jana Jijini Dar e Salaam ikiwa katika msafara wa kitaifa kati ya Serikali ya Oman na Tanzania.
Aidha, katika tukio hilo Mh. Waziri DK. Kigwangalla aliweza kuungana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Mama Samia Suluhu Hassan katika chakula cha mchana ndani ya Meli hiyo ya Mfalme wa Oman Mhe. Qaboos bin Said  ijulinakanyo kama ‘Fulk Al Salamah’.

Meli hiyo ya kifahari ya Mfalme wa Oman Mhe. Qaboos bin Said ‘Fulk Al Salamah’ ipo nchini hadi Oktoba 21.2017. ambapo ipo nchini kusambaza ujumbe wa ‘Amani na upendo’ duniani ambapo  ikitoka Tanzania  inatarajia kuelekea Mombasa Kenya kwa madhumuni hayo hayo.

No comments:

Post a Comment