Monday 30 October 2017

IEBC kumtangaza Rais wa Kenya

  Kenya. Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatarajiwa kutangaza matokeo ya uchaguzi wa marudio kwa kura ya utais uliofanyika Oktoba 26 na kutangaza ikiwa itaandaa uchaguzi katika majimbo 25 ambako uliahirishwa.
Makamu wa Rais wa tume hiyo, IEBC, Consolata Nkatha alisema jana jioni kwamba walikuwa wamepokea matokeo kutoka majimbo sita kati ya saba yaliyokuwa yamesalia na kwamba kufikia Jumatatu asubuhi matokeo yote yatakuwa yamejumlishwa.
“Tumepokea matokeo kutoka majimbo sita sasa na tutakuwa katika nafasi ya kutangaza matokeo ya mwisho kesho (leo) asubuhi. Tutafanya kazi usiku kucha kuhakikisha uhakiki na ujumlishaji unakamilika. Pia tutatangaza ikiwa tutaendesha uchaguzi katika majimbo 25 ambako uliahirishwa au la,” alisema Nkatha.
Majimbo hayo yaki kwenye kaunti ambazo tume iliahirisha uchaguzi ambazo ni Kisumu, Migori, Siaya na Homa Bay.
Mawasiliano na IEBC yamekuwa haba lakini inafahamika kwamba makamishna wa tume walifanya kikao cha saa kadhaa na wanasheria wao juzi kufikiria kama wajaribu kuitisha uchaguzi katika majimbo 25.
Jana jioni Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alisema tume yake ilikuwa imehakiki matokeo ya majimbo 259 kati ya 265, yakiwemo ya nchi za nje.
Kutoka katika majimbo hayo, Chebukati alisema watu 7,447,014 walijitokeza kupiga kura sawa na asilimia 43.04. Matokeo yaliyokuwa yakitangazwa moja kwa moja kutoka jengo la Bomas of Kenya Rais Kenyatta alijikusanyia kura 7,393,405 sawa na asilimia 98.3 ya kura halali.

Wagombea wengine wote wamepata kura chini ya 100,000 akiwemo Raila Odinga aliyejiondoa japokuwa amepigiwa kura 70,425.

No comments:

Post a Comment