Friday, 20 October 2017

Korea Kaskazini yaionya Australia

Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un

Serikali ya Australia imesema kuwa imepokea stakhabadhi kutoka Korea Kaskazini ikiitaka Canbera kutojihusisha na utawala wa rais Trump.
Barua hiyo imeshutumu onyo la Marekani kwamba itaiangamiza Korea Kaskazini iwapo italazimika kujilinda.
Waziri mkuu wa Australia PM Malcolm Turnbull amesema kuwa barua hiyo pia ilitumwa kwa mataifa mengine.
Amesema inaonyesha kuwa shinikizo za kidiplomasia dhidi ya Korea Kaskzini zimeanza kufanya kazi, licha ya barua hiyo kuwa na ufyozi na malalamishi ya kawaida ya taifa hilo.
Barua hiyo yenye ukurasa mmoja ilitumwa kupitia ubalozi wa Korea Kaskazini nchini Indonesia na inadaiwa kutoka kwa kamati ya maswala ya kigeni ya Korea Kaskazini.
Imezitaka serikali nyengine kujitenga na hatua zisizokuwa na heshima za rais Trump ikisisitiza kuwa Marekani inaweza kusababisha janga kubwa la kinyuklia.
Bwana Turnbull amesema kuwa Korea Kaskazini ndio inayosababisha wasiwasi kwa kutishia kuyashambulia mataifa ya Japan, Korea Kusini na Marekani kwa kutumia silaha za kinyuklia.
''Wametuma barua hizi kwa mataifa mengi , kama barua iliosambazwa'', alisema Bwana Turnbull kwa kituo kimoja cha redio 3AW.
Waziri wa maswala ya kigeni Julie Bishop aliitaja barua hiyo kuwa hatua isiokuwa ya kawaida ya Korea Kaskazini.
Baadaye bwana Turnbull alionekana kutojali umuhimu wake akiifananisha na ufyozi na malalamishi kuhusu Donald Trump unaotolewa na Korea Kaskazini.
Hatahivyo wote wanakubaliana kwamba huenda ni ishara kwamba shinikizo za kimataifa dhidi ya taifa hilo zimeanza kuzaa matunda na kuwa na matumaini kwamba kutakuwa na majadiliana ya kimataifa.
Siku ya Jumamosi Pyonyang iliionya Australia kwamba haitaweza kuzuia janga iwapo itashirikiana na sera za Marekani dhidi ya utawala wa Kim Jong Un.
Korea Kaskazini imekiuka makubaliano ya kimataifa katika miezi ya hivi karibuni kupitia kufanyia majaribio kombora lake la kinyuklia mbali na kurusha makombora mawili juu ya anga ya taifa la Japan.

Marekani imejibu kwa vitisho vya kijeshi , lakini waziri wa maswala ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson anasisitiza kuwa bwana Trump yuko tayari kuutatua mgogoro huo kupitia diplomasia.

No comments:

Post a Comment