Saturday, 28 October 2017
Udart yapata hasara
Mvua kubwa iliyonyesha jijini Dar es Salaam kwa siku mbili imesababisha kampuni ya Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) kuhamisha baadhi ya shughuli eneo la Jangwani.
Mbali ya kuathiri shughuli katika eneo hilo, Udart imesema mvua iliyonyesha Jumatano Oktoba 25 na Alhamisi Oktoba 26,2017 imesababisha mabasi 29 ya kampuni hiyo kuharibika.
Udart imehamisha huduma za kulaza magari, ujazaji wa mafuta na gereji.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Udart, Deus Bugaywa amesema leo Jumamosi Oktoba 28,2017 kuwa vituo vya Gerezani na Kimara ndivyo vitatoa huduma ya gereji.
Amesema vituo vya Kivukoni, Gerezani na Kimara vitatoa huduma ya kulaza magari na kuyajaza mafuta.
Bugaywa amesema mvua imeathiri mabasi 29 kati ya 134 yanayotoa huduma jijini Dar es Salaam.
Amesema vifaa vya mabasi vimesombwa na maji na pia baadhi ya vyumba vya ofisi vimeharibiwa.
"Kwanza, tunawaomba msamaha wateja kwa usumbufu uliojitokeza Alhamisi wakati wa mvua. Kwa sasa watuvumilie hadi Jumapili Oktoba 28,2017 huduma zitakaporejea vizuri. Mabasi 29 yalishindwa kuendelea na huduma baada ya kuathiriwa na mvua," amesema Bugaywa akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema, "Mabasi hayo yalikuwa kwenye marekebisho katika injini, giaboksi na difu. Mvua zilipoanza maji yalijaa na matengenezo yalisimama. Kwa sasa mafundi wanaangalia athari na namna gani zishughulikiwe mapema ili magari yarudi barabarani."
Bugaywa amesema kwa sasa si rahisi kuwa na makadirio ya hasara iliyotokana na mvua.
Alipoulizwa kuhusu hatima ya kutumia majengo ya ofisi yaliyopo Jangwani, Bugaywa amesema suala hilo linahitaji majadiliano kati ya Serikali na wadau wote wanaohusika katika mradi huo.
"Tutakaa na wadau wote, Udart ni sehemu tu ya wadau, kwa hiyo tutakaa tuone ni kwa namna gani tunazuia au tunapunguza hasara kutokana na mvua," amesema Bugaywa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment