Mkurugenzi wa Compass
Communications ambaye pia ndiye mwandaaji mkuu wa mashindano haya Maria
Sarungi Tsehai (Kulia) akisisitiza jambo wakati wa kikao na Baraza la
Sanaa Tanzania (Basata).Anayesikiliza Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa na
Masoko wa Basata, Vivian Shalua na Afisa Sanaa, Bona Leon Masenge.
Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa na
Masoko wa Basata, Vivian Shalua (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja
na Miss Univerese mwaka jana, Jihan Dimachk (Kulia) na Miss Earth
Tanzania, Lilian Loth.
Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa na
Masoko wa Basata, Vivian Shalua (wanne kutoka kulia) akiwa katika picha
ya pamoja na warembo, waandaaji na maofisa wa Basata mara baada ya
kumalizika kikao cha pamoja cha kujadili mashindano hayo.
Na Mwandishi wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (Basata)
limeipongeza kampuni ya Compass Communications Tanzania kwa kufanya
mashindano bora ya Miss Universe hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi
wa Ukuzaji Sanaa na Masoko wa Basata, Vivian Shalua wakati wa kufanya
tathimini ya mashindano hayo na mashindano ya urembo kwa ujumla.
Mrembo Jihan Dimachk alishinda
taji la Miss Universe mwaka jana huku Lilian Loth akishinda nafasi ya
pili katika mashindano hayo.
Shalua alisema Basata wamefarijika
sana na jinsi mashindano hayo yanavyoendeshwa na hakuna malalamiko
yoyote kuhusiana na zawadi na upendeleo.
Alisema kuwa kutokana na utaratibu
mzuri wa mashindano yao, Basata imeridhia waandaaji wa mashindano hayo,
kufanya mashindano ya mwaka huu na vile vile kuandaa mashindano ya
kutimiza miaka 10 tokea kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 2007.
“Pamoja na kuwa na shindano moja
kwa kushirikisha warembo wa mikoa tofauti, bado Basata imefarijika na
jinsi mnavyoendesha na utaratibu unaotumia kuwapata warembo, uendeshaji
wa mashindano mpaka kumpata mshindi,”
“Tunajua kuwa kuna changamoto za
wadhamini na kusababisha kufanya mashindano yenye kalenda fupi na
kuondoa mlolongo wa matukio, hatua hii ni bora zaidi ili kuondoa
malalamiko ya zawadi na mambo mengine, huu ni mfano wa kuigwa,” alisema
Shalua.
Mkurugenzi wa Compass
Communications ambaye pia ndiye mwandaaji mkuu wa mashindano haya Maria
Sarungi Tsehai aliishukuru Basata kwa usimamiaji bora wa mashindano
katika sekta ya sanaa nchini na kusema kuwa watajihidi kuongeza wigo ili
kuona warembo wengi zaidi kutoka mikoa tofauti wanashiriki katika
mashindano yao.
Maria alisema kuwa pamoja na
changamoto zote wanazokabiliana nazo, bado wanahitaji msaada kutoka
Basata ili kupata wadhamini na kufikia malengo yao katika kuendeleza
Sanaa hapa nchini.
“Kwa sasa kuna changamoto kubwa ya
wadhamini wa mashindano, kuna haja ya kupata msaada kutoka Basata ambao
ni chombo cha serikali, mnaweza kutusaidia kupata wadhamini hata kwa
Wizara ya Maliasili na Utalii, sisi tunatangaza jina la nchi na utalii
pia, tunaamini kupitia kwenu, tunaweza kupata sapoti kubwa kutoka wizara
hiyo, Bodi ya Utalii (TTB) na mamlaka ya zake kama Tanapa,” alisema
Maria.
No comments:
Post a Comment