Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama
akiongea baada ya ziara ya ya kutembelea kiwanda cha kuzalisha bidhaa za
ngozi pamoja na kuangalia maendeleo ya ujenzi wa kiwanda kipya eneo la
Karanga Moshi Mkoani Kilimajaro ambapo aliipongeza PPF pamoja na Jeshi
la Magereza kwakufanya maamuzi sahihi yanayoendana na dira ya Serikali
ya awamu ya tano ya kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda kwa kuja na
mradi wa uboreshaji na ujenzi wa kiwanda kipya cha kuzalisha bidhaa za
ngozi cha Karanga Moshi Mkoani Kilimanjaro.(Picha na: MAELEZO)
Na: Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama
ameipongeza bodi ya wadhamini ya Mfuko wa Pensheni wa PPF kwa uamuzi wa
kushirikiana na Jeshi la Magereza katika kujenga kiwanda kipya pamoja na
kuendeleza kiwanda cha Bidhaa za ngozi Karanga Kilichopo Mkoani
Kilimanjaro.
Akizungumza wakati wa ziara ya
kutembelea na kuona maendeleo ya kiwanda hicho Waziri Mhagama amesema
kuwa PPF na Jeshi la Magereza wamefanya maamuzi sahihi yanayoendana na
dira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa na uchumi wa kati kupitia
viwanda.
“Dhamira ya Serikali ni kufikia
uchumi wa kati kupitia viwanda, PPF na Jeshi la Magereza mmeonesha
mfano, uboreshaji wa kiwanda hiki na ujenzi wa kiwanda kingine ambacho
kitakuwa na viwanda vidogovidogo vinne ni ishara ya kutimia kwa ahadi ya
Rais wetu Dkt. John Magufuli ya kuwa na uchumi wa kati kupitia
Viwanda”. Alisema Mhe. Jenista.
Aidha, alisema kuwa lengo la
Serikali ni kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa kiwango cha
kuridhisha na Serikali itatoa msaada popote inapohitajika ili kwa haraka
nchi yetu ianze kuzalisha viatu ambavyo vitauzwa nje ndani na nje ya
nchi hatimaye kuliingizia taifa mapato.
Akizungumzia kuhusu ajira
zitakazozalishwa na kiwanda hicho Waziri Mhagama amesema kuwa kiwanda
hiki pekee kitatoa ajira za moja kwa moja 689 na zisizo za moja kwa moja
1800 hivyo kusaidia kukabiliana na changamoto ya ajira hasa kwa vijana
nchini.
Naye Waziri wa Fedha na Mipango
Dkt. Philip Mpango amesema kuwa PPF na Jeshi la Magereza lazima
wahakikishe mipango waliyoiweka ya ujenzi wa kiwanda kipya na maboresho
ya kiwanda cha zamani yanafanyika kwa wakati ili kwa haraka uzalishaji
uanze na hatimaye nchi iweze kunufaika.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi Mhe. Mhandisi Hamad Masauni ameishauri mifuko mingine ya pesheni
kutumia fursa zilizopo Jeshi la Magereza ikiwamo maeneo na rasilimali
watu katika kufikia azama ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa na uchumi
wa kati kupitia viwanda.
Akiongelea ujenzi wa kiwanda
kipya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni za wastaafu PPF, Bw.William
Erio amesema kuwa kiwanda hicho kitagharimu shilingi bilioni 54.4 na
kitakuwa na uwezo wa kuzalisha na wanategemea kuzalisha futi mraba za
ngozi Milioni tatu laki saba na nusu (3,750,000/=) kwa mwaka.
Vilevile Bw. Erio amesema kuwa
kiwanda hicho kitazalisha viatu vya kijeshi na kiraia jozi milioni moja
na laki mbili kwa mwaka, pamoja na kutoa soli laki tisa kwa mwaka pamoja
na kutoa bidhaa nyingine za ngozi kama mikanda,mabegi na mikoba ya
akina mama takribani elfu arobaini na nane kwa mwaka.
No comments:
Post a Comment