Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na
Uzalishaji Mkoa wa Singida Beatus Chowaji akisoma bango mara baaa ya
kuzindua mradi wa Faida Mali unaoshirikiana na shirika la AMDT katika
kuwasaidia wakulima wa Alizeti Singida.
Mkurugenzi wa Shirika la AMDT
Michael Kayombo akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa Faida Mali
wenye lengo la kuwasaidia wakulima wa Alizeti Singida kulima kibiashara.
Baadhi ya wadau waliohudhuruia
uzinduzi wa mradi wa Faida Mali wenye lengo la kuwasaidia wakulima wa
Alizeti Singida kulima kibiashara.
Mkurugenzi wa mradi wa Faida Mali
mkoa wa Singida Tom Silayo akisoma taarifa ya mradi huo kwa wajumbe
waliohudhuria uzinduzi wa mradi utakaowasaidia wakulima kulima alizeti
kibiashara.
Mtendaji Mkuu wa Chama cha
wasindikaji wa Mbegu za alizeti Tanzania Daud Musa Mwasantaja
akiwahakikishia wakulima wa alizeti upatikanaji wa soko katika uzinduzi
wa Mradi wa Faida Mali.
Wauzaji wa pembejeo ambao sio
waaminifu wamepewa onyo kali na endapo atabainika yeyote anayewalaghai
wakulima na kuwauzia pembejeo ambazo sio hali hatua kali dhidi yake
zitachukuliwa.
Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na
Uzalishaji Mkoa wa Singida Beatus Chowaji ametoa onyo hilo wakati
akizindua mradi wa Faida Mali unaoshirikiana na shirika la AMDT katika
kuwasaidia wakulima wa alizeti Mkoani Singida ili kulima zao hilo
kibiashara zaidi.
Chowaji amesema kumekuwepo na
malalamiko kwa baadhi ya wakulima ambao hukumbana na wauzaji wa pembejeo
ambao sio waaminifu na kuwalaghai kwakuwa wakulima hao hawana elimu na
uelewa hasa wa viuatilifu au mbegu ambazo ni halisi.
Ameongeza kuwa mkono wa serikali
ni merfu na utawabaini popote walipo hivyo waache mara moja kwani kwa
kufanya hivyo wanakirudisha nyuma kilimo cha alizeti ambacho ni tegemeo
kwa ajili ya uchumi wa viwanda Mkoani Singida.
“Singida tuna Viwanda vya kuamua
mafuta ya alizeti vikubwa viwili, vya kati vitatu na vidogo 115 na
kufanya jumla ya viwanda vya alizeti kuwa 120, vyote hivyo vinategemea
alizeti ya mkulima, lakini pia mkulima anakuwa na matarajioa makubwa,
hao wauzaji pembejeo wasio waaminifu hatutawavumilia, tena waache mara
moja”, amesisitiza Chowaji.
Aidha amelipongeza shirika la
AMDT kupitia mradi wa Faida mali kwa kuuchagua Mkoa wa Singida ili
kuboresha kilimo cha alizeti hasa kwa ajili ya mkulima mdogo.
Chowaji amesema viwanda vya
alizeti Mkoani Singida hufanya kazi kwa miezi minane kwa mwaka badala ya
mwaka mzima kutokana na kuwa alizeti inayozalisha bado haitosheleshi
viwanda hivyo kufanya kazi mwaka mzima.
Amesema matumaini makubwa ya
serikali mkoani hapa ni kuwa mradi huo utasaidia kuongeza uzalishaji wa
zao hilo ili kuifanya Singida ya Viwanda kuwa bora zaidi pamoja na
kuliboresha zao lenyewe la alizeti kwa kutumia pembejeo za kisasa zaidi.
Chowaji amewataka wakulima wote
wa alizeti kuchangamkia fursa hiyo kwa kujiunga katika vikundi ili
waweze kufikiwa kwa urahisi na kunufaika, pia waache kilimo cha mazoea
kwakuwa alizeti ni biashara kubwa ambayo itawakomboa kiuchumi na kukupa
pato la mkoa wa Singida.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Shirika la AMDT Michael Kayombo amesema shirika hilo kupitia Mradi wa
Faida mali utahakikisha unasaidia upatikanaji wa mikopo kwa wakulima
wadogo wa alizeti Mkoani singida.
Kayombo ameongeza kuwa mradi
utaboresha huduma za ugani kwa kutoa taarifa sahihi na mapema juu ya
kilimo cha alizeti kwa wakulima na taarifa hizo zitatolewa kwa njia ya
ujumbe mfupi wa maneno hivyo kuwafikia mapema.
Amreongeza kuwa watahakikisha
wakulima wanapata soko la uhakika la zao hilo ndani na nje ya mkoa wa
singida pamoja na kuhakikisha bei ya zao hilo ni yenye kumnufaisha
mkulima na sio kumdidimiza zaidi.
Naye Mtendaji Mkuu wa Chama cha
wasindikaji wa Mbegu za alizeti Tanzania Daud Musa Mwasantaja amesema
viwanda vya alizeti bado vina uhitaji mkubwa wa alizeti kwa kuwa viwanda
vyao vimekuwa vikiendeshwa chini ya malengo kutokana na mbegu hizo kuwa
chache.
Mwasantaja amesema wana imani
kuwa mraadi wa Faida Mali utasaidia kuongeza uzalishaji wa alizeti hivyo
kuwasaidia kuongeza pia uzalishaji katika viwanda vyao.
Ameongeza kuwa watatoa
ushirikiano wa kutosha na hivyo wakulima wasiwe na wasiwasi walime zao
hilo kwa wingi watapata wateja na kwa bei ambayo ni nzuri.
Nao wakulima walioshiriki
uzinduzi wa maradi huo wamesema mradi huo umekuja muda muafaka kwakuwa
na wao wanatamani kupata faida kutokana na kilimo hicho kwakuwa baadhi
bado wanalima kwa mazoea na kwa kutumia mbegu ambazo hazizalishi kwa
wingi.
No comments:
Post a Comment