



Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Wataalam wa masuala ya maji
kutoka nchi 25 za Bara la Afrika wamekutana kujadili njia
zitakazowezesha upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini
ifikapo mwaka 2030.
Mkutano huo umefunguliwa leo
Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson
Lwenge ambaye amesema kuwa majadiliano hayo yameanzishwa baada ya
azimio la Umoja wa Mataifa Namba 6 kuzitaka nchi zote Duniani
kuhakikisha kuwa wananchi wao wanapata huduma ya maji safi na salama
ifikapo mwaka huo.
“Ili kuhakikisha agizo la Umoja
wa Mataifa linatekelezwa, nchi za Umoja wa Afrika ziliamua kuunda kamati
za wataalam watakaojikita katika kupanga mikakati endelevu ya
kutekeleza agizo hili,”alisema Mhandisi Lwenge.
Mhandisi Lwenge ameongeza kuwa
baada ya majadiliano hayo wataalam watapeleka taarifa katika kikao cha
Baraza la Mawaziri wa Maji Afrika (AMCOW) kinachotegemewa kufanyika
mwezi Septemba mwaka huu ili kuweza kupata tathmini ya kila nchi namna
inavyotekeleza azimio hilo.
Aidha, Mhandisi Lwenge amefafanua
kuwa kwa miaka mitano ijayo, Tanzania imejipanga kuhakikisha kuwa
wananchi wanaokaa mijini wanapata maji safi na salama kwa asilimia 95 na
vijijini asilimia 85, uondoaji wa maji taka kwa asilimia 30 pamoja na
kuhakikisha nyumba za vijijini zina vyoo.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji
wa AMCOW, Dkt. Conisius Kanangire amesema kuwa mkutano huo
umewashirikisha wataalam pamoja na wadau kutoka mashirika mbalimbali
yanayohusika na uangalizi wa mabonde ya maziwa na mito Afrika ili nao
waweze kutoa mchango wa mawazo utakaopelekea nchi za Afrika kuwa na
maendeleo makubwa katika sekta ya maji.
”Baraza la Mawaziri wa Maji pekee
haliwezi kuleta mafanikio makubwa tunayoyataka kwa Afrika ndio maana
tumeamua kuwashirikisha wataalam wa maji kutusaidia namna ambavyo
tutaweza kuwa na mikakati mizuri ambayo itawezesha upatikanaji wa maji
safi na salama kwa nchi zote,” alisema Dkt. Kanangire.
Dkt. Kanangire ameishkuru
Serikali ya Tanzania kwa kushiriki bega kwa bega katika kuhakikisha
baraza hilo linafanya kazi nzuri hivyo anategemea kuwa kikao hicho
kinachoendelea nchini kitatoa majibu ya uhakika juu ya upatikanaji wa
maji safi na salama.
No comments:
Post a Comment