Makamu Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Albert Msole akiomba
ridhaa ya kuchaguliwa tena kushikilia nafasi hiyo kwenye baraza la
madiwani ambapo alichaguwa tena kwa mwaka 2017/2018 na madiwani hao
Makamu Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Albert Msole (CCM)
amefanikiwa kushinda tena nafasi hiyo baada ya kumbwaga mpinzani wake
Philemon Oyogo (Chadema).
Mkurugenzi mtendaji
wa halmashauri ya wilaya hiyo, Yefred Myenzi akitoa matokeo hayo alisema
kati ya madiwani 22 waliopiga kura, madiwani 14 walimpigia Msole na
madiwani nane walimpigia Oyogo.
Myenzi alisema Msole
atadumu kwenye nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja wa 2017/2018
ndipo utakapofanyika uchaguzi mwingine wa makamu Mwenyekiti.
Akizungumza baada ya
kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi hiyo Msole aliwashukuru madiwani wote
kwa heshima kubwa waliyompa na kumrudishia tena nafasi hiyo hivyo
ataendelea kushirikiana nao kuhakikisha kuwa halmashauri hiyo inasonga
mbele kwenye maendeleo.
“Tuendelee
kushirikiana pamoja kwani tumeshirikiana vizuri tangu mwaka 2015 na kazi
yangu kubwa ni kumsaidia Mwenyekiti wa halmashauri yetu, natoa ahadi
kwenu kuwa nitaendelea kuteleleza wajibu wangu kwani heshima mliyonipa
ni kubwa japo mimi ni mdogo kwenu,” alisema Msole.
Mwenyekiti wa
halmashauri hiyo Jackson Sipitieck alisema kama siyo jambo la kisheria,
kanuni na taratibu, wasingeruhusu uchaguzi huo ufanyike kwani jitihada
za Msole za uchapakazi kwenye halmashauri hiyo zinajulikana.
“Msole ni mpambanaji
mzuri, muwajibikaji, muwazi na anayefanya kazi zake kwa kutenda haki
bila kupendelea mtu na nadhani wote tunatambua jitihada zake kama siyo
sheria angekuwa makamu Mwenyekiti kwa miaka yote mitano,” alisema
Sipitieck.
Alitangaza wajumbe
wa kamati ya fedha, uongozi na mipango ni Alamayan Ranga na Grace
Mtataiko, Mwenyekiti wa kamati ya uchumi, ujenzi na mazingira, Loishiye
Lesakwi na Mwenyekiti wa kamati ya jamii, Sendeu Laizer.
Aliwataja wajumbe wa
kamati ya maendeleo ya jamii ni Julius Mamasita, Ngaidiko Tipai,
Philemon Oyogo, Haiyo Mamasita, Michael Haiyo, Nyika Shawishi na Ezekiel
Lesenga Mardadi.
Alisema wajumbe wa
kamati ya uchumi ni Lucas Moringe, Christopher Kuya, Saimon Kikoda,
Naishorwa Tunay, Paulina Makeseni, Rehema Namani, Thomas Yohana na Diana
Kuluo.
No comments:
Post a Comment