Na Neema Mathias – MAELEZO
Chama cha Walemavu Tanzania
(CHAWATA) kimeiomba Serikali kuondoa kodi kwa bajaji (pikipiki zenye
magurudumu matatu) zinazotumiwa na watu wenye ulemavu kama miguu na pia
kubeba abiria ili kujipatia kipato.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa
CHAWATA John Mlabu mapema leo Jijini Dar es Salaam, alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto na ajira kwa watu
wenye ulemavu.
“Kupitia fursa ya kuondolewa kodi
kwa vifaa vya watu wenye ulemavu tunaiomba Serikali izitambue bajaji
kuwa ni moja ya nyenzo inayomsaidia mtu mwenye ulemavu na hivyo
ziondolewe kodi, na Serikali iziagize kwa wingi na kuzikabidhi kwa watu
wenye ulemavu kwa mkopo kupitia Umoja wa Waendesha Bajaji Dar es Salaam
(UWAWABADA),” amesema Mlabu.
Ameendelea kwa kusema, kupitia
UWAWABADA bajaji hizo zitatawanywa kote nchini kwa utaratibu walionao
ili ziwainue kiuchumi na kuboresha maisha yao na familia zao.
Aidha Mlabu amesema, CHAWATA
kinamuomba Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake kuangalia
kundi hilo kupitia mafanikio ya watu wenye ulemavu Jijini, Dar es Salaam
na kurasimisha shughuli ya uendeshaji wa bajaji kuwa ya watu wenye
ulemavu pekee na wengine wasio na ulemavu waendeshe pikipiki za kawaida
(Bodaboda).
“Kuendesha Bajaji ni ajira pekee
ambayo haina usumbufu kwetu na imeyagusa makundi yote ya wanawake na
wanaume tena rika zote, maana kwenye ujenzi wa viwanda na makampuni sisi
hatuajiriwi, licha ya uwepo wa sheria Na. 9 ya 2010 ya ajira kwa
walemavu inayotaka kila mahali pa kazi 3% ya watumishi wake wawe watu
wenye ulemavu,” amefafanua Mlabu.
Vile vile amesema, uwepo wa chombo
hicho cha magurudumu matatu kimewasaidia sana walemavu kujipatia kipato
na kuwaondoa katika maisha ya kuombaomba kama ilivyokuwa hapo awali,
aidha amesema kuwa wanaichangia Serikali katika kukuza uchumi wa nchi
kupita kodi mbalimbali za Serikali pale wanaponunua mafuta ama vipuli
vya bajaji zao.
CHAWATA kimeipongeza Serikali ya
Awamu ya Tano na Rais Dkt. Magufuli kwa kujali watu wa tabaka la chini
na maskini katika Taifa hili, ambapo wameshuhudia mara nyingi katika
ziara zake akiwatetea wafanyabiashara wadogo (Machinga), Wakulima na
Wafugaji, hivyo wanamuona Rais Magufuli kuwa ni Rais wa wanyonge.
No comments:
Post a Comment