Serikali ya Uganda inafanya juhudi za kubadilisha Katiba ya nchi hiyo na
kuondoa kipengele kinachoweka ukomo wa umri wa mtu kuwania urais na
hivyo kumuandalia mazingira Rais Yoweri Museveni aendelee kuitawala
nchi hiyo.
Akizungumzia suala hilo mjini Kampala Mshauri wa Rais, David Mafabi
amesema kuwa kuna juhudi zinafanyika ili kuondoa kipengele hicho na
hivyo kumfanya Rais Museveni awanie tena kiti cha urais katika uchaguzi
ujao.
Hilo ni jaribio jingine la kumfanya Rais Museveni aendelee kuitawala
Uganda baada ya mwaka 2005 kufanyika marekebisho ya Katiba yaliyoondoa
kifungu kinachoweka ukomo wa rais kuongoza kwa mihula miwili.
Katiba ya Uganda inaeleza kuwa, mtu haruhusiwi kuwania urais akiwa na
miaka 75, lakini pia inaeleza kuwa umri wa anayetaka kuwania urais ni
lazima uwe 35 na kuendelea.
Wabunge wa chama tawala nchini Uganda cha NRM wanaounga mkono
marekebisho hayo wanadai kuwa, sheria hiyo ya ukomo wa umri ikiendelea
kuwepo itakuwa kikwazo kwa raia wa nchi hiyo wenye umri mkubwa lakini
wenye uwezo wa kuendelea kuongoza nchi hiyo.
Mpango huo unaonekana wazi kuwa, unalenga kumuandalia mazingira Rais
Museveni kuwania tena urais mwaka 2021, atakapokuwa na umri wa miaka 76
ameitawala nchi hiyo tangu mwaka 1986.
Tayari vyama vya upinzani nchini Uganda vimetangaza kuupinga mpango huo.
Kizza Besigye, kiongozi mkongwe wa upinzani nchini uganda amewata
wananchi wa nchi hiyo kuyakataa marekebisho hayo ya katiba.
No comments:
Post a Comment