Balozi John Kijazi
Watanzania wametakiwa kujiwekea utaratibu wa kuangalia
afya zao mara kwa mara ili kuhakikisha wakati wote afya zinakuwa salama.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatatu, Julai 17 na Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi John Kijazi akiwa ni mmoja wa waombolezaji waliofika kwenye msiba
wa mke wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison
Mwakyembe, Linah Mwakyembe aliyefariki dunia juzi usiku kutokana na
ugonjwa wa saratani ya titi.
Sanjari na hilo, Balozi Kijazi amewasisitiza Watanzania kuwa na
utamaduni wa kufanya mazoezi ili kujiweka mbali na magonjwa
yasiyoambukiza.
Amesema Watanzania wengi wanapoteza maisha kutokana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo saratani.
"Ni muhimu kufanya vipimo mara kwa mara, ikitokea umebainika kuwa na
ugonjwa ni rahisi kuupatia matibabu ukiwa kwenye hatua za awali,"
amesema.
"Tatizo linapogundulika mapema ni rahisi kuokoa maisha ya mgonjwa tena
kwa gharama nafuu za matibabu kinyume na hapo gharama zinakuwa juu na
kupona inakuwa bahati," amesisitiza.
No comments:
Post a Comment