Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akisalimiana na Mkuu wa
Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Tellack, mara baada ya kuwasili mkoani humo
kwa ziara ya kikazi.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akifafanua jambo kwa
viongozi wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara alipokutana nao mkoani humo
kwa ziara ya kikazi.
Muonekano wa jengo la Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga ambalo limekamilika na ujenzi wake
umesimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akikagua moja ya nyumba za watumishi
eneo la Rubaga zinazojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), mkoani
Shinyanga.
Muonekano wa jengo la Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ambalo ujenzi wake unasimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Meneja wa Wakala wa Majengo
Tanzania (TBA), mkoa wa Shinyanga Eng. Amosi Manyete akimuonesha Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, mfumo wa maji
taka uliowekwa nje ya jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania, kanda ya
Shinyanga iliyopo mkoani humo. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu,
Kanda hiyo Mhe. Jaji Richard Kibella.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameutaka Wakala wa Majengo Tanzania
(TBA), kuhakikisha ndani ya miezi sita wanakamilisha ujenzi wa nyumba ya
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga.
Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo
mkoani humo wakati alipokagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wakala
huo ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza umuhimu wa kuwapatia
waheshimiwa majaji mahali pazuri pa kuishi ili waweze kutimiza wajibu
wao wa kutenda haki kwa wananchi ipasavyo.
“Hakikisheni mnakamilisha ujenzi
wa nyumba hii haraka iwezekanavyo ili Mheshimiwa huyu apate mahali
pazuri pa kuishi, kufanya hivi kutarahisisha majukumu yake na kufanikish
utendaji wa kazi”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amesisitiza umuhimu wa Wakala huo
kuongeza kasi katika miradi mbalimbali inayoendelea ya ujenzi wa nyumba
za viongozi ili kuondoa adha ya kodi za pango kubwa zinazopotea kwa
viongozi hao kupanga kwa watu binafsi.
Naye, Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu, Kanda ya Shinyanga Mhe. Jaji Richard Kibella amemshukuru Prof.
Mbarawa kwa niaba ya taasisi zake za TBA na Wakala wa Ufundi na Umeme
(TEMESA), kwa namna ambavyo wameshirikiana na Mahakama kukamilisha
ujenzi wa jengo hilo na kuwapatia huduma nyingine za uendeshaji.
Aidha, ameiomba Serikali
kukamilisha kwa haraka ujenzi wa nyumba za viongozi na watumishi wa
mahakama kwani gharama kubwa zinatumika katika malipo ya upangaji wa
nyumba za viongozi.
“Mhe. Prof. Mbarawa suala la
nyumba ni changamoto, nyumba za kupanga zina gharama kubwa ambapo kwa
namna moja au nyingine inaongeza gharama za uendeshaji wa mahakama na
kupunguza usalama”, amefafanua Jaji Kibella.
Kwa upande wake Mtendaji wa
Mahakama hiyo Bwana Ernest Masanja, amemueleza Prof. Mbarawa kuwa
kukamilka kwa jengo la Mahakama hiyo kumewezesha Majaji na watendaji
wengine wa mahakama kufanya kazi kwa bidii, ufanisi na kwa wakati katika
kuwapatia wananchi haki.
Katika hatua nyingine, Prof.
Mbarawa ametembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Hospitali
ya Mkoa huo unaosimamiwa na TBA na ameuelekeza Wakala huo kushirikiana
na Mamlaka husika kuhakikisha kuwa ujenzi wake unazingatia viwango na
ubora na kukamilika kwa wakati.
No comments:
Post a Comment