Wafanyakazi 260 wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Mji wa Dodoma (CDA) wamepangiwa vituo vipya vya kazi.
Kwa mujibu wa Waziri Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene wafanyakazi 150 kutoka kundi hilo
wanabaki Manispaa ya Dodoma huku wengine 66 wakipelekwa katika
halmashuri na mikoa mbalimbali nchini.
Amesema wafanyakazi 16 wamepelekwa Tamisemi, DART (14), Hospitali ya
Benjamini Mkapa Dodoma (4), Chuo Kikuu cha Dodoma (3), Ofisi ya Waziri
Mkuu (3), Wizara ya Ardhi (2) Ofisi ya Bunge (1) na Utumishi wa Umma
(1).
Waziri Simbachawene amewataka wafanyakazi hao kuripoti katika vituo vyao
vya kazi mara baada ya kupata barua na Serikali haitasita kufuta ajira
ya mtumishi yeyote ambaye atakaidi agizo hilo.
Rais wa John Magufuli aliivunja rasmi CDA Mei mwaka huu na kuagiza mali
na shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na CDA zihamishiwe Halmashauri
ya Manispaa ya Dodoma.
Rais Magufuli amesema ameamua kuivunja CDA na kuhamishia majukumu yake
katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ili kuondoa mkanganyiko wa
utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema mkanganyiko huo ulikuwa ukisababishwa na mgongano kati ya vyombo hivyo viwili.
Aidha, amesema mahitaji ya sasa yamedhihirisha kuwa hakuna haja ya kuwepo kwa CDA.
“Wananchi wa Dodoma wamelalamikia tatizo hili kwa muda mrefu, hata
nilipokuwa kwenye kampeni zangu za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015
walilalamika sana, sasa nimetekeleza niliyowaahidi,” amesema Dk
Magufuli.
“Naamini kwa uamuzi huu malalamiko ya wananchi yatapata utatuzi na pia
tutakuwa tumeondoa kikwazo cha umiliki wa muda mfupi wa ardhi
uliosababisha wawekezaji kushindwa kujenga viwanda Dodoma.
CDA ilianzishwa kwa Amri ya Rais ya Aprili Mosi, 1973 na kutangazwa kupitia tangazo la Serikali namba 230.
No comments:
Post a Comment