Friday 14 July 2017

Mazingira kabumbu Cup

1 (2)
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga akiwa na baadhi ya askari Mgambo wakiwa wanashiriki katika moja ya  zoezi la kufanya usafi (PICHA NA VICTOR MASANGU)

NA VICTOR  MASANGU, BAGAMOYO
MKUU  wa Wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga katika kuunga juhudi za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dk. John Magufuli katika kukuza michezo hapa nchini ameamua kuandaa mashindano maalumu ya mchezo wa soka ambayo yatazishiriikisha jumla ya timu  28 kutoka   kata  26 zilizopo Wilayani humo yaliyopewa kwa jina la ‘Mazingira kabumbu Cup 2017’.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Majid alisema kwamba  Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi lake Julai 15 katika uwanja  wa Mwanakalenge ambapo  lengo kubwa na kuanzisha mashiindano hayo ni kwa ajili ya kuweza  kuwakutanisha vijana  na viongozi mbali mbali  wa serikali pamoja na wabunge,na  madiwani  katika kuwahimiza suala zima la utunzaji wa mazingira sambamba na kushiriki kikamilifu katika kufanya usafi.
Pia alifafanua kuwa katika mashindano hayo pia  yatawajumisha  viongozi wengine wa   serikali kutoka idara mbali mbali  pamoja na kuwashirikisha  madiwani na wabunge  wote kutoka halmashauri  zote mbili za  Bagamoyo pamoja na  Chalinze  ili kuweza kushiriki katika mashindano hayo ambayo yatakwenda sambamba na  kuweka mikakati kabambe ya kuweza kutunza vyanzo vya maji,kutunza afya,pamoja na  mazingira.
“Kitu kikubwa  ninachopenda kukisema ofisi ya Mkuu wa Wilaya tumeona ni vema kumuunga mkono Rais wetu wa awamu ya tano John Magufuli katika kutunza na kufanya usafi wa mazingira sambamba na agizo la Makamu wa Rais la Mama Samia Suluhu  Hassan la kufanya mazoezi  ya michezo kila mwisho wa mwezi tumeamua kuandaa michuano hiyo ambayo itajulikana kama Mazingira kabumbu Cup 2017,”ambayo itaenda sambamba na zoezi la kufanya  usafi wa mazingira.
Majid alibainisha kuwa mshindi  wa kwanza katika mashindano hayo atajinyakulia zawadi ya Piki piki ya matairi matatu aina ya Toyo ambayo  pia itaweza kutumika katika shughuli mbali mbali za kuweza  kusaidia kwa kiasi kikubwa  kusombea taka taka kwa lengo la kuweza kuyaweka mazingira katika hali ya usafi .
Aidha alisema kwamba ana imani  kwamba kufanyika kwa mashindano hayo Wilayani Bagamoyo  kutaweza kuwapa fursa wachezaji wengine  ambao walikuwa hawapati fursa ya  kuweza kuonyesha vipaji vyao walivyonavyo katika kulisakata kabumbu.
Katika hatua nyingine Majid alisema kwamba katika mchezo wa  ufunguzi wa mashindano hayo utazikutanisha timu ya madiwani ambao wataungana na wabunge  wote waili  kutoka  halmashauri zote mbili za Chalinze na bagamoyo ambao watamenyana vilivyo na timu  ya wakuu wa idara kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
 
Pia Majid aliwaomba wadau wa mchezo wa kabumbu pamoja na wananchi wa Wilayanai Bagamoyo kujitokeza kwa wingi siku hiyo kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika zviwanja hivyo vya Mwanakalenge pamoja na kujitokeza katika kufanya usafi wa mazingira katika maeneo mbali mbali ili kuweza kutekeleza agizo la Rais Dk.John Magufuli.

No comments:

Post a Comment