Amesema mkataba huo si wa haki na unahatarisha mamilioni ya nafasi za kazi za watu wa Marekani.
Kujitoa katika mkataba huo ilikua ni mojawapo ya ajenda wakati wa kampeni za Trump
Bw Trump amesema yuko tayari kuanzisha mashauriano ya mkataba mpya au airejeshe Marekani baadaye katika mkataba huo chini ya masharti yaliyoimarishwa.
Lakini amesema kuwa yeye hawezi kuunga mkono makubaliano ambayo - kwa matamshi yake mwenyewe - yanaadhibu Marekani bila kuwawajibisha wachafuzi wakubwa wa mazingira, ambapo amezitaja China na India.
Bw Trump amesema wakati wa kampeni za urais mwaka jana, aliahidi kwamba angechukua hatua kusaidia sekta za mafuta na makaa yam awe nchini Marekani.
Wapinzani wake wanasema kujiondoa kwenye Mkataba huo ni sawa na Marekani kuyakimbia majukumu yake kama kiongozi katika kukabili changamoto hiyo inayoikabili dunia.
Mkataba wa Paris unaitaka Marekani na nchi nyingine 187 kudhibiti ongezeko la viwango vya joto duniani kuhakikisha kiwango cha joto kinafikia nyuzijoto 2C chini ya kiwango kilichokuwepo kabla ya mageuzi ya kiviwanda, na baadaye kukipunguza zaidi hadi nyuzijoto 1.5C.
Ni Syria na Nicaragua pekee ambazo zilikataa kutia saini mkataba huo.
Akihutubu katika bustani ya White House Rose, Bw Trump amesema mkataba huo wa Paris unalenya kuidhoofisha na kuifanya Marekani kuwa nchi maskini.
Amedai mkataba huo utaigharimu Marekani $3tn ya mapato na nafazi za kazi 6.5 milioni - huku mataifa yanayoshindana na Marekani kama vile China na India yakifaidi.
"Ili kutimiza wajibu wangu wa kuilinda Marekani na raia wake, Marekani itajiondoa kutoka kwa Mkataba wa tabia nchi wa Paris ….lakini itaanza mashauriano ya kujiunga tena na mkataba huo wa Paris au mkataba mwingine mpya kabisa kwa masharti ambayo ni nafuu kwa Marekani," alisema.
Kwenye hotuba yake, alikariri baadhi ya maneno aliyokuwa akiyasema kwenye kampeni.
"Hatutaki viongozi wengine na nchi nyingine ziwe zinatucheka tena - hilo halitafanyika," alisema.
"Nilichaguliwa kuwawakilisha raia wa Pittsburgh, na si wa Paris. Niliahidi ningejitoa au kushauriana upya kuhusu mkataba wowote ambao haujali maslahi ya Marekani. Mikataba mingi ya kibiashara itaanza kujadiliwa upya karibuni."
Mwandishi wa BBC Rajini Vaidyanathan mjini Washington anasema hatua hiyo ya Bw Trump itashangiliwa sana na wengi wa wafuasi wake, wengi ambao hawajali sana kuhusu sayansi na mazingira.
Wachanganuzi wanasema kujiondoa kwa Marekani kutoka kwa Mkataba wa Paris kutaifanya vigumu kwa ulimwengu kutimiza malengo yaliyowekwa katika mkataba huo.
Marekani huchangia 15% ya gesi kaboni duniani, lakini pia ni mfadhili mkubwa kifedha na kiteknolojia wa mataifa yanayostawi katika juhudi za mataifa hayo kukabiliana na ongezeko la joto duniani.
No comments:
Post a Comment