Sunday, 25 June 2017

Uongozi wa Yanga nao walaani kitendo cha mashabiki kuchoma jezi ya Niyonzima

 Uongozi wa Yanga umelaani kitendo cha mashabiki wachache wa Yanga kuchoma jezi namba nane iliyokuwa inavaliwa na kiungo Haruna Niyonzima.
Wiki iliyopita, Yanga kupitia Katibu wake Mkuu, Charles Boniface Mkwasa ilitangaza rasmi kumuachia Niyonzima raia wa Rwanda kuendelea na maisha yake.
Yanga ilisema imejitahidi kukaa meza moja na Niyonzima, lakini dau lake limekuwa kubwa na mwisho wamemuachia aendelee na maisha yake na mwisho wakamtakia kila la kheri.
Siku chache baada ya kauli hiyo, ikaonekana baadhi ya mashabiki wakichoma jezi za kiungo huyo Mnyarwanda wakionyesha hasira zao kutokana na uamuzi wake wa kuamua kuondoka na kwa kuwa ameanza mazungumzo na Simba.

"Si sahihi, huwezi kuchoma jezi ya mtu eti kisa kaondoka, Niyonzima si mchezaji wa kwanza kuondoka au kujiunga na Yanga. Mashabiki wanapaswa kujitambua na kuelewa mchezo wa soka uko vipi, sisi tunaona hili si jambo la kiungwana," alisema Mkwasa.

Hata kabla ya ungozi wa Yanga kutamka kuhusiana na tukio hilo, baadhi ya mashabiki wa Yanga ambao wengi wanajitambua pia walilaani tukio hilo na kuliita ni la "kishamba".


No comments:

Post a Comment