23/06/2017
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tunapoelekea kipindi hiki cha
sikukuu ya Eid El Fitri, Jeshi la Polisi nchini, linatoa tahadhari kwa
wananchi kuwa makini katika suala zima la ulinzi na usalama wa maisha na
mali zao. Kipindi kama hiki cha sikukuu baadhi ya watu hupenda kutumia
fursa hiyo kufanya vitendo vya uhalifu na vitendo vingine ambavyo
huhatarisha usalama wa watu na mali zao.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi
nchini, limejipanga kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na
usalama katika mikoa yote kuhakikisha kwamba wananchi wanasherehekea
Sikukuu katika hali ya amani na utulivu.
Aidha, ulinzi umeimarishwa
kwenye maeneo yote, yakiwemo maeneo ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu
za starehe na maeneo mengine ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya
watu.
Vilevile, Jeshi la Polisi
linawatahadharisha watumiaji wa vyombo vya moto barabarani kuwa makini
na kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, Jeshi la Polisi
halitasita kuwachukulia hatua kwa wale wote watakaovunja sheria na
kanuni za usalama barabarani kwa mabereva kutumia vilevi, bodaboda
kubeba mishikaki, kwenda mwendo kasi pamoja na kupiga honi hovyo.
Pia, tunawataka wananchi wote
kuwa wepesi katika kutoa taarifa kwa kupitia namba za simu za bure
111 au 112 pindi wanapoona viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo
yao ya makazi ama maeneo ya biashara.
Tunawatakia watanzania wote Sikukuu njema ya Eid El Fitri.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba -ACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Jeshi la Polisi
No comments:
Post a Comment