Meneja Uendeshaji wa Multichoice Tanzania Baraka Shelukindo akikabidhi mashuka kwa Mlezi wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Al-Madinnah kilichopo Tandale jijini Dar es Salaam Kuruthum Juma (wa pili kulia). Wa pili Kushoto ni Malkia wa Taarabu Hadija Kopa na kulia ni Muigizaji maarufu wa tamthilia ya Huba Riyama Ali ambao ni mabalozi maalum wa DStv. Hafla hiyo iliyofanyika mapema leo katika kituo hicho ambapo vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni mbili vikiwemo vyakula, mashuka, vyombo na mitungi ya kuzimia moto vilikabidhiwa
Watoto wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Almadinnah kilichopo Tandale wakipokea vyombo kutoka kwa Meneja Uendeshaji wa Multichoice Tanzania Baraka Shelukindo baada ya kupokea msaada wa vyakula na vifaa mbalimbali kutoka kampuni hiyo jana.
Mshonaji katika mradi wa ushonaji
wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Al-Madinnah cha Tandale jijini
Dar es Salaam Aziza Amri (wa pili kulia) akitoa maelezo kuhusu mradi huo
unaofadhiliwa na kampuni ya Multichoice Tanzania. Kutoka kushoto ni
Malkia wa mipasho Hadija Kopa ambaye ni balozi maalum wa DStv,
BiKuruthum Juma ambaye ni mkuu wa kituo hicho, Baraka Shelukindo Meneja
Uendeshaji wa Multichoice Tanzania na kulia ni Muigizaji maarufu wa
tamthilia ya Huba Riyama Ali. Mbali na kutembelea mradi huo, Multichoice
pia ilikabidhi vyakula na vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi
milioni mbili kwa kituo hicho
Kampuni ya Multichoice Tanzania
imetoa zawadi ya sikukuu ya Idi kwa kituo cha kulelea watoto yatima cha
Al-Madinnah kilichopo Tandale jijini Dar es Salaam. Msaada huo wa
vyakula na vifaa mbalimbali umekabidhiwa kwa kituo hicho na Meneja
Uendeshaji wa Multichoice Tanzania Baraka Shelukindo katika hafla fupi
iliyofanyika kituoni hapo ambayo pia ilihudhuriwa na mabalozi kadhaa wa
DStv akiwemo malkia wa Taarab Khadija Kopa na muigizaji maarufu wa
filamu na Tamhtilia ya HUBA , Riyama Alli.
Akizungumza wakati wa
kukabidhi zawadi hizo, Shelukindo amesema kwa takriban miaka mitano
mfululizo Multichoice imekuwa ikikisaidia kituo hicho kwa mambo
mbalimbali. Amesema wanafanya hivyo kwa kutambua kuwa malezi ya watoto
waishio katika mazingira magumu ni jukumu la kila mtu na kila taasisi.
“Tunatambua kuwa jukumu la kuwalea watoto kama hawa ambao kwa sababu
moja ama nyingine wamejikuta katika mazingira magumu ni letu sote. Hawa
ni ndugu zetu, watoto wetu, na pia ni tegemeo kubwa kwa taifa letu,
hivyo kuwasaidia ni jukumu letu”
Amesema mbali na kwamba
Multichoice imekuwa ikikisaidia kituo hicho mara kwa mara kwa kuwapa
vyakula na mahitaji mengine, lakini pia waliamua kufadhili uanzishwaji
wa mradi wa ushonaji ambao unakisaidia kituo hicho katika kujiingizia
kipato. “Tunajua kuwa chakula, malazi na mambo mengineyo ni muhimu kwa
maisha ya kila siku ya vijana wetu, lakini pia tuliona ni busara
kuwawekea kamradi japo kadogo ambako wataweza kujipatia kipato.
Tumefurahi sana kuona mradi huu unaendelea na tunaamini kuwa wataweza
kuuendeleza na kuukuza ili uwasaidia Zaidi.” Alisema Shelukindo.
Kwa upande wake Mkuu wa kituo
hicho Mama Kuruthum Juma ameishukuru Multichoice Tanzania kwa msaada
wao wa mara kwa mara kwa miaka mingi sasa. Amesema kitendo cha
Multichoice Tanzania kukisaidia kitua hicho kwa mambo mbalimbali hususan
mradi wa ushonaji kumewasaidia sana katika kujipatia kipata japo
kusaidia gharama za uendeshaji kituo hicho ambazo ni kubwa. “Kwa kweli
gharama za uendeshaji kituo ni kubwa sana na kama mnavyofahamu watoto
wanaolelewa hapa hawana uwezo na wengi wao hawana wazazi, hivyo ni
jukumu letu kuwalea, kuwapa matibabu, na pia kuwasomesha, hili kwa kweli
ni jukumu kubwa na tunahitaji msaada kutoka kwa wadau mbalimbali”
alisema Mama Kuruthum
Amesema idadi ya watoto
imekuwa ikiongezeka lakini kituo hakina uwezo mkubwa kutokana na ufinyu
wa eneo na bajeti hivyo akawaomba wadau wengine kuangalia uwezekano wa
kukisaidia kituo hicho ili kiweze kuhudumia watoto wengi Zaidi.
Naye Malkia wa Taarabu –
Khadija Kopa amesema amefarijika sana kuona Multichoice Tanzania
inawajali watoto hususan wale waishio katika mazingira magumu ambao
aghalabu husahaulika na jamii. “Kwakweli Multichoice Tanzania wamefanya
jambo la maana sana. Ni vyema tukaunganisha nguvu zetu kuwalea hawa
watoto wetu kwani nao wana haki kama watoto wengine” alisema Kopa.
Naye muigizaji Riyama Ali
amepongeza jitihada zinazofanywa na Multichoice Tanzania pamoja na
uongozi wa kituo cha Almadinna katika kuwasaidia watoto hao. “Watoto
hawa ni hazina ya taifa. Tukiwasaidia hawa wakakua vizuri, wakapata
elimu nzuri, kesho na keshokutwa tutapata wabunge humu, mawaziri,
wakurugenzi, wanamichezo, wasanii na kadhalika. Tushirikiane kuwalea na
hili ni jukumu letu sote na ni kitu kinacholeta Baraka” alisema Riyama.
Kituo cha Al-Madinnah
Orphanage Centre kilianzishwa mwaka 2004 na kwa hivi sasa kituo hicho
kinahudumia jumla ya watoto 65 ambapo 40 kati yao ni wavulana na 25
wasichana na wengi wao ni wanafunzi wa shule za msingi.
No comments:
Post a Comment