Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemtaka Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge pamoja na watendaji wake kuhakikisha
Mji wa Kisarawe uliopo mkoani Pwani unapata huduma ya maji safi na
salama.
Rais Dkt. Magufuli ametoa
agizo hilo jana mkoani Pwani wakati akizindua Mradi wa upanuzi wa Mtambo
wa maji wa Ruvu Juu na ulazaji wa Mabomba Makuu kutoka Mlandizi kwenda
Jijini Dar es Salaam.
Mh. Magufuli amesema kuwa Mkoa wa
Pwani umefanya kazi kubwa ya kutunza miundombinu ya maji ambayo
imewezesha kuhudumia wananchi wa Dar es Salaam hivyo ni haki kwa
wananchi wa Mkoa huo kufaidika na maji wanayoyatunza kwa muda mrefu.
“Ninafahamu Mji wa Kibaha kwa
sasa hauna shida ya maji, shida iliyopo ni kuzidi kwa presha ya maji
ambayo sio tatizo la DAWASA wala DAWASCO hivyo ili kutatua tatizo hilo
ni jukumu la Wizara husika na watendaji wake kujipanga na wahandisi wa
maji kuunganisha bomba kutoka Wilaya ya Kibaha hadi Kisarawe ambapo kuna
changamoto ya maji safi na salama,” alisema Rais Magufuli.
Akiongelea utunzaji wa
miundombinu ya maji, Rais Dkt. Magufuli amewataka watendaji wa Wizara ya
Maji na Umwagiliaji kuhakikisha wanashughulikia maji yanayopotea kwa
kurekebisha miundombinu ambayo imeharibika na kuweka miundo mbinu mipya
inayoweza kuhimili wingi wa maji.
Aidha, Rais Magufuli ameishukuru
Serikali ya India kwa kutoa trilioni 1.3 kwa ajili ya kuendeleza miradi
ya maji kwa Miji 16 nchini ambayo ikikamilika itawezesha wananchi wengi
kupata maji safi na salama hivyo amewaahidi kudumisha ushirikiano uliopo
katika sekta ya maji baina ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake Waziri wa Maji
na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema kuwa Mradi huo ni sehemu
ya miradi mikubwa saba ya kimkakati inayoendelea kupanuliwa ikiwemo ya
upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini, Ruvu Juu, Uchimbaji visima virefu,
Ujenzi wa bwawa la Kidunda, upanuzi wa mtandao wa usambazaji maji, mradi
wa kupunguza upotevu wa maji na uboreshaji wa mfumo wa majitaka.
“Mradi huu umejengwa na fedha za
mkopo jumla ya shilingi bilioni 87 kutoka Serikali ya India kupitia
Benki ya Exim ambapo umesaidia pia kujenga nyumba 17 za wafanyakazi
katika eneo la mradi,” alisema Mhandisi Lwenge.
Mhandisi Lwenge amefafanua kuwa
baada ya upanuzi huo mashine zinauwezo wa kuvuta maji kati ya lita
milioni 182 – 196 kwa siku hivyo hadi kufikia mwezi Machi, 2016 wananchi
742,611 wa mkoani Pwani wanapata maji safi na salama.
Nae Balozi wa India nchini
Tanzania, Sandeep Arya amesema kuwa uhusiano wa sekta ya maji kati ya
Tanzania na India ulianza miaka 35 iliyopita na maji ndiyo sekta ya
kipaumbele inayounganisha Tanzania na India hivyo uhusiano baina ya nchi
hizo ni wa kindugu.
“Uamuzi wa kutoa mkopo wa shilingi
Trilioni 1.1 kwa ajili ya mradi wa usambazaji maji katika Miji 17
nchini Tanzania unaendelea kudhihirisha ushirikiano wetu,” alisema
Balozi Arya.
Uzalishaji wa sasa wa mitambo yote
unafikisha jumla ya lita Milioni 502 kwa siku ambazo ni majumuisho ya
maji ya Ruvu Juu lita milioni 196, Ruvu chini lita milioni 270 pamoja na
mtambo mdogo wa Mtoni unaozalisha kiasi kidogo kwa siku.
No comments:
Post a Comment