Meneja ujenzi wa kampuni ya BAM
International, Bw. Rey Blumrick akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa wa hatua iliyofikiwa
kwenye ujenzi wa Jengo la 3 la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere, wakati Waziri huyo alipokagua ujenzi wa
jengo hilo leo mchana.
Meneja ujenzi wa kampuni ya BAM
International, Bw. Rey Blumrick akifafanua Jambo kwa Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (Katikati), wakati
Waziri huyo alipokagua ujenzi wa Jengo la 3 la Abiria katika Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa nne kushoto), akiwa katika
pichaa ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania (TAA), na watendaji mbalimbali mara baaada ya kukagua ujenzi wa
Jengo la 3 la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere, leo mchana.
Muonekano wa sehemu ya Jengo la 3
la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Kukamilika kwake kutawezesha jengo hilo kuhudumia abiria wapatao milioni
8 na nusu kwa mwaka.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amekagua ujenzi wa jengo la Tatu la
Abiria la uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), na
kuelezea kuridhishwa kwake kwa hatua ya ujenzi iliyofikiwa.
Akizungumza mara baada ya kukagua
ujenzi huo Waziri Profesa Mbarawa amemhakikishia mkandarasi BAM
International anayejenga jengo hilo kuwa Serikali italipa madai yake kwa
wakati kwa kadri atakavyoyawasilisha.
“Nia yetu ujenzi huu ukamilike
ifikapo Septemba mwakani, hivyo tunamtaka mkandarasi kuongeza kasi ya
ujenzi na wasimamizi kumsimamia kikamilifu ili vifaa vinavyofungwa
katika jengo hilo viwe na ubora uliokusudiwa na vidumu kwa muda mrefu”,
amesisitiza Profesa Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesema kukamilika
kwa jengo la tatu la abiria la uwanja wa ndege wa Julius Nyerere
kutawezesha uwanja huo kuweza kuhudumia abiria wapatao milioni 8 na
nusu kwa mwaka na hivyo kukuza uchumi wa nchi kwa kuwezesha watalii na
wageni wengi zaidi kufika nchini.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri
ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Profesa Ninatubu Lema
amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa ujenzi huo unasimamiwa
kikamilifu na utamalizika kwa wakati.
“Kama wasimamizi tumejipanga
kuhakikisha zoezi la ufungaji vifaa katika jengo hili, linakamilika kwa
wakati na kwa ubora unaotakiwa,” amesisitiza Prof. Lema.
Naye Meneja ujenzi wa BAM International, Bw. Rey Blumrick amesema kazi iko katika hatua nzuri na itakamilika kwa wakati.
Mradi wa ujenzi wa jengo la tatu
la abiria ni sehemu ya uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere lengo likiwa ni kuwezesha ndege na abiria wengi kutumia
uwanja huu na kuhuisha sekta ya usafiri wa anga hapa nchini.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment