Frank Mvungi-Maelezo
Jeshi la Polisi Kikosi cha
Usalama Barabarani limetoa tahadhari kwa watumiaji wote wa barabara
nchini kuzingatia sheria ili kuepuka ajali hususani wakati wa sikukuu ya
Eid el Fitri.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo
vya habari iliyotolewa leo Jijini Dar es Salaam na Kaimu Kamanda Kikosi
cha Usalama Barabarani Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP)
Fortunatus Musilimu uzoefu umeonyesha kuwa katika kipindi cha sikukuu
madereva wamekuwa wakiendesha magari kwa mwendo kasi, kuyapita magari
mengine bila kuchukua tahadhari na kubeba abiria kupita kiasi hali
inayoweza kusababisha ajali.
“Tutafanya operesheni kali
barabarani, kuwapima madereva kiwango cha ulevi na watakaobainika
wamelewa watakamatwa na kuwekwa mahabusu na kufikishwa mahakamani,
nasisitiza kwamba,dereva anayetaka kuendesha gari asinywe pombe,akitaka
kunywa pombe asiendeshe gari” alisisitiza Kamishna Musilimu katika
taarifa hiyo.
Aidha taarifa imewatahadharisha
wamiliki wa magari yatakayokodishwa kwenda maeneo ya Fukwe bila kibali
kuwa yatakamtwa na wahusika kufikishwa mahakmani.
Pia alitoa wito kwa wazazi
kuangalia usalama wa watoto wao na wasiwaache wakatembea peke yao
barabarani bila uangalizi ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
Kwa upande wa madereva wa
Pikipiki (Bodaboda) amesema kuwa nao wamekuwa wakipita taa
nyekundu,wakiendesha pikipiki zao bila kuvaa kofia ngumu,kubeba abiria
zaidi ya mmoja (mishikaki) na abiria hao kutovaa kofia ngumu hivyo
kuhatarisha Usalama wao.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Jeshi
la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limekuwa likihamasisha na
kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na matumizi
sahihi ya barabara ili kuepuka ajali katika kipindi chote na hasa wakati
huu wa sikukuu.
No comments:
Post a Comment