Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi
Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald Rwakatare akiwasili katika
Kituo Kikuu cha Mabasi Yaendayo Haraka cha Kimara Mwisho. Mhandisi
Rwakatare alipokewa na Kaimu Meneja Usafirishaji wa Wakala wa Mabasi
Yaendayo Haraka Dkt Philemon Mzee (kushoto).
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi
Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald Rwakatare akipita sehemu ya
ukaguzi wa tiketi na kadi zitumiwazo na Mabasi Yaendayo Haraka. Mhandisi
Rwakatare alipata fursa ya kutembelea vitengo mbalimbali vya Kituo
Kikuu cha Kimara mwisho na kujionea huduma za usafiri zinavyofanyika
katika kituo hicho.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi
Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald Rwakatare akizungumza na mmoja
wa abiria wa Mabasi yaendayo haraka katika Kituo Kikuu cha Mabasi hayo
katika eneo la Kimara Mwisho.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi
Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald Rwakatare (kulia) akitembelea
vitengo mbalimbali vya kutoa huduma katika Kituo Kikuu cha Mabasi
yaendayo haraka kilichopo Kimara mwisho. Mhandisi Rwakatare aliambatana
na Kaimu Meneja Usafirishaji wa DART Dkt Philemon Mzee, na Kushoto ni
Afisa Habari Mkuu wa DART bwana Mathew Kwembe.
Sehemu ya daraja linalotumiwa na
wananchi pindi wanapoingia na kutoka katika Kituo Kikuu cha Mabasi
Yaendayo Haraka kilichopo Kimara Mwisho. Daraja hili ni miongoni mwa
miundombinu iliyojengwa na Serikali kwa ushirikiano na Benki ya Dunia.
Na Mathew Kwembe
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi
Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald Rwakatare ameeleza kuwa mradi
huo umepata mafanikio makubwa katika kupunguza msongamano wa magari
jijini Dar es salaam hususani katika barabara ya Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa
habari mara baada ya kutembelea kituo kikuu cha Kimara mwisho ikiwa ni
sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma, Mhandisi Rwakatare
alisema kuwa katika kipindi hicho cha mpito, Mabasi yaendayo haraka
yameweza kusafirisha watu 200,000 kila siku kutoka watu 50,000 iliyokuwa
ikisafirisha mwaka jana, wakati mradi unaanza.
Mhandisi Rwakatare alieleza kuwa
Mradi huo umeweza kuokoa muda wa wananchi ambao kabla ya mradi kuanza
walikuwa wakitumia usafiri mwingine uliokuwa ukichukua kutoka masaa
mawili, wakati sasa wanatumia dakika 45 tu kwa safari ya kutoka Kimara
hadi Posta kwa kutumia mabasi yaendayo haraka.
Alifafanua kuwa huduma hiyo mbali
na kuwapunguzia mzigo wa nauli watumiaji wa kawaida wa mabasi ya
daladala, mradi wa mabasi yaendayo haraka imeokoa gharama ya usafiri kwa
wenye magari binafsi ambapo wengi wao wamekuwa wakiutumia zaidi usafiri
huo.
Akizungumzia kuhusu maadhimisho
ya wiki ya utumishi wa umma Mhandisi Rwakatare alisema kwa wakala umeona
ni vyema kutumia maadhimisho hayo kusikiliza kero na maoni ya wananchi
hasa watumiaji wa huduma hiyo ili kuona namna nzuri ya kuiboresha.
“Watumishi wa Wakala wa Mabasi
yaendayo haraka wamekuwepo katika vituo vya Gerezani na Kimara mwisho
kwa siku hizi mbili ili kusikiliza kero na maoni kutoka kwa wananchi
wetu, na tunafurahi kuona huduma hii ikizidi kushika kasi, hasa kwa
kuzingatia kuwa tupo katika kipindi cha mpito,” alisema.
Hata hivyo alisema kuwa maoni na
ushauri walioupata kutoka kwa wananchi wataufanyia kazi na kurekebisha
kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika kipindi cha mpito ili
kuhakikisha kuwa huduma hiyo inakuwa bora zaidi.
Aisema kuwa Wakala upo mbioni
kumpata mtoa huduma ya ukusanyaji mapato ambapo ndiye atakuwa na jukumu
la kushughulikia suala la kadi ili kuondokana na changamoto mbalimbali
za usafiri zinazowakabili watumiaji wa mabasi hayo.
“Natambua kuwa kadi zimeisha na
wakala unalishughulikia jambo hili na tutahakikisha kuwa tunaongeza
kadi, nawasihi wananchi watambue kuwa tupo katika kipindi cha mpito,
mapungufu mengi yaliyojitokeza tutayarekebisha,” alisema.
Mhandisi Rwakatare alibainisha
kuwa suala la kadi limechukua muda mrefu kwa vile mchakato wake
unahusisha mfumo wa kibenki na hivyo kuwataka wananchi wa jiji la Dar es
salaam kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha mpito kutokana na
changamoto mbalimbali zilizojitokeza hususani suala la kadi ambapo
aliahidi kulitafutia ufumbuzi suala hilo mapema iwezekanavyo.
Mhandisi Rwakatare alisema kuwa
Mradi huo unatekelezwa kwa ubia baina ya Serikali na Kampuni binafsi ya
UDART ambayo ndiyo iliyopewa jukumu la kutoa huduma ya usafiri wa mabasi
yaendayo haraka katika kipindi hiki cha mpito
Alisema Serikali kwa upande wake
imeshirikiana na Benki ya Dunia kujenga miundombinu mbalimbali
inayotumiwa na mabasi hayo ambapo katika awamu ya kwanza ujenzi wake
umehusisha barabara zenye jumla ya kilometa 20.9 ambazo ni Kimara –
Kivukoni, Magomeni – Morocco na Faya – Karikaoo.
Pia alisema kuwa Wakala wa Mabasi
yaendayo haraka upo mbioni kumpata mtoa huduma kamili baada ya kipindi
cha mwaka mmoja cha mpito. Alisema kuwa Wakala unatarajia kuongeza
mabasi mengine 165 kwa ajili ya kutoa huduma zaidi za usafiri katika
jiji la Dar es salaam.
Alisema kuwa wakala unatarajia kuongeza njia za mrisho katika maeneo ya Mwenge, Kawe na Mabibo.
Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka
ulianza rasmi tarehe 16 Mei, 2016, ambapo umekwishatimiza mwaka mmoja
katika kipindi cha mpito tangu kuanza kutolewa kwa huduma hiyo ambapo
zimepangwa awamu sita za ujenzi wa miundombinu ya mradi huo katika
maeneo mengine ya jiji la Dar es salaam huku awamu ya kwanza
imekwishakamilika
No comments:
Post a Comment