Benjamin Sawe,Maelezo
Jamii imetakiwa kuwapa umuhimu
watoto wa kike na kuachana na mtazamo potofu kuwa hawana mchango mkubwa
kwa jamii, hali inayochangia utumikishwaji wa watoto na kujiingiza
katika mahusiano ya kimapenzi na biashara ya ngono katika umri mdogo.
Hayo yemesemwa na Kamishna wa
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Kamishna Salma Ali Hassan
katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana.
Kamishna Salma amesema
Vitendo hivyo vimekuwa chanzo cha mimba na ndoa za utotoni ambazo
huwaletea madhara mbalimbali ikiwemo: unyanyasaji wa kimwili,
kisaikolojia, kingono, athari za kiafya, vifo wakati wa
ujauzito/kujifungua na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU).
“Wakati tunaadhimisha siku hii
muhimu wadau wote wa haki za watoto hatuna budi kujitathimini namna
tunavyowaandaa watoto wetu ili waweze kutoa mchango stahiki katika
maendeleo ya Taifa letu”.Alisema Kamishana Salma.
Alisema Tanzania ni miongoni
mwa nchi zilizochukua hatua mbalimbali kuhakikisha uwepo wa maslahi ya
watoto. ikiwa ni pamoja na kutunga sheria na kuridhia mikataba
mbalimbali ya kimataifa na kikanda inayolinda na kutetea haki za mtoto.
Alisema Mikataba hiyo inajumuisha,
Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto (1989), Tamko la Shirika
la Kazi Duniani (ILO) Na. 182, na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa
Mtoto (2003).
“Miongoni mwa sheria
zilizotungwa katika ngazi ya kitaifa ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania (1977), Sheria ya Mtoto Na. 21/2009, Sheria ya Kanuni za
Adhabu, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na Sheria ya Makosa ya
Kujamiiana – SOSPA (1998)”. Alisema Kamishana Salma.
Pia Serikali imeridhia na
kubuni sera, mipango na mikakati mbalimbali ya kitaifa na kimataifa,
ikiwemo: Sera ya Mtoto (2008), na Mpango-kazi wa Kitaifa wa Kuzuia na
Kupambana na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (2017- 2022).
Alisema Kimataifa Serikali
imeridhia na inatekeleza Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ya Dunia
(SDG’s) yaliyopitishwa mwaka 2015 yanayobainisha kuwa watoto wana haki
ya kuishi, kulindwa, kutobaguliwa na kushirikishwa kwa usawa ili
kuhakikisha kuwa wanapata fursa sawa katika jamii.
Juhudi hizo ni muhimu kipindi hiki
katika kuunga mkono dhamira ya Serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. John Pombe Magufuli katika
kuhakikisha kuwa Tanzania inafikia azma yake ya “Kujenga Tanzania ya Viwanda.”
Alisema Pamoja na jitihada
zote bado zipo changamoto mbalimbali zinazoathiri malezi ya watoto na
kuwanyima fursa katika jamii, changamoto hizo ni pamoja na: umaskini,
migogoro ya wanandoa, mila potofu, utandawazi, majukumu ya kijinsia
katika jamii na ukosefu wa haki ya elimu ya afya ya uzazi (reproductive
and health rights).
Tume inaitaka jamii kuwapa
umuhimu watoto wa kike na kuachana na mtazamo potofu kuwa hawana mchango
mkubwa kwa jamii, hali inayochangia utumikishwaji wa watoto na
kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na biashara ya ngono katika
umri mdogo.
Siku ya Mtoto wa Afrika
huadhimishwa kimataifa kote duniani kwa lengo la kutambua thamani, utu
na umuhimu wa mtoto duniani. Maadhimisho haya hufanyika Juni 16 kila
mwaka tangu ilipotangazwa rasmi na jumuiya ya Umoja wa Afrika mnamo
mwaka 1991.
No comments:
Post a Comment