Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihutubia kwenye Tamasha la
Uelimishaji na Upimaji Afya na Kinga dhidi ya Magonjwa yasiyoambukiza
kwa watoto na vijana kwenye uwanja wa michezo wa shule ya msingi
Kinyerezi.Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais
Na Jacquiline Mrisho- MAELEZO
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi
kuwafichua watu wanaonyanyasa na kudhalilisha watoto kijinsia ili
wachukuliwe hatua za kisheria.
Mhe. Samia ameyasema hayo leo
Jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha kampeni ya kudhibiti magonjwa
yasiyo ya kuambukiza pamoja na maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika
katika viwanja vya Shule ya msingi Kinyerezi vilivyopo jijini humo.
Vile vile amesema, watu wanaofanya
vitendo vya udhalilishaji wa watoto wapo miongoni mwa jamii hivyo ni
jukumu la Serikali, walezi na wazazi kuwafichua watenda maovu hao ili
kukomesha vitendo hivyo na kuwafanya watoto waishi kwa amani nchini.
”Katika kukabiliana na hali hiyo,
nimeviagiza vyombo vya dola kutofumbia macho vitendo hivyo pindi
wanapopata taarifa za matukio ya udhalilishaji wa watoto na badala yake
wachukue hatua za haraka za kuwakamata na kuwachukulia hatua stahiki
watu wanaofanya vitendo hivyo vibaya,” alisema Mhe. Samia.
Makamu wa Rais ameongeza kuwa
kufanya hivyo kutawasaidia watoto kuwa salama katika mazingira ya
nyumbani hata wakiwa mashuleni kwani watu wabaya wanaofanya vitendo
hivyo watawajibishwa kulingana na matendo maovu wanayoyafanya watoto.
Aidha, Makamu wa Rais ametoa wito
kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kote nchini kuwapatia
taarifa Walimu wao na Polisi ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali
za kisheria.
Siku ya Mtoto wa Afrika
huadhimishwa kimataifa kote duniani kwa lengo la kutambua thamani, utu
na umuhimu wa mtoto duniani. Maadhimisho haya hufanyika Juni 16 kila
mwaka tangu ilipotangazwa rasmi na jumuiya ya Umoja wa Afrika mnamo
mwaka 1991.
No comments:
Post a Comment