Jovina Bujulu – MAELEZO
Desemba
9, mwaka huu Tanzania itatimiza miaka 55 ya Uhuru ambao ulipatikana
mwaka 1961, chini ya uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K.
Nyerere.
Maadhimisho ya Uhuru kwa mwaka huu yanashuhudia kukua na kupanuka kwa wigo wa vyama vya siasa nhini.
Vyama
vya siasa ni nguzo muhimu katika ujenzi wa demokrasia na ujio wake
umeongeza elimu na maarifa ya siasa kwa wananchi, ambapo wanashiriki kwa
kiwango kikubwa katika siasa katika ngazi zote.
Ushuhuda
wa kukua kwa demokrasia unajidhirisha katika ushiriki wa vyama vya
siasa katika chaguzi mbali mbali kuanzia ngazi za chini hadi juu.
Historia
inaonyesha kwamba Tanganyika (Tanzania kwa sasa) ilifanya uchaguzi wake
wa kwanza mwaka 1962, ambapo kulikua na vyama viwili vya siasa ambavyo
ni TANU kilichokua kinaongozwa na Mwalimu Nyerere na chama cha African
National Congress (ANC) kilichokua kinaongozwa na Zuberi Mtemvu.
Baada
ya uchaguzi huo wa mwaka 1962 Tanganyika ikawa taifa la chama kimoja
cha siasa (TANU). Wakati huo utaratibu wa uchaguzi uliokuwapo ni kamati
Tendaji ya TANU kuchagua watu wawili na kuwapeleka kwa wapiga kura ili
kumpata Mbunge na nafasi ya urais ilihusika jina moja lililokuwa
linachaguliwa na mkutano mkuu wa TANU na ASP.
Mfumo huo ulitumika katika chama tawala yaani chama kimoja ambapo uchaguzi ulifanyika mwaka 1965,1970,1975 mpaka 1990.
Mwaka
1992, Tanzania iliingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa
mujibu wa sheria ya vyama vya siasa namba 5 na mwaka 1995 uchaguzi wa
kwanza chini ya mfumo huo wa vyama vingi ulifanyika ikawa ni miaka
thelathini na tatu tangu uchaguzi wa kwanza uliohusisha vyama viwili
ulipofanyika mwaka 1962.
Mfumo
wa vyama vingi vya siasa ni hali ya kuwa na chama zaidi ya kimoja
katika nchi moja. Madhumuni ya mfumo huo ni katika nchi yoyote ni kuleta
ushindani wa kisiasa ili kuleta maendeleo ya nchi na kuongeza wigo wa
demokrasia katika nchi husika.
Akizungumzia chimbuko la mfumo huu nchini,
Ndugu John Tendwa ambaye aliwahi kuwa msajili wa vyama vya siasa nchini
alisema kuwa “Kulikuwa na vugu vugu la wanajamii la kuleta msukumo
katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, ambao uliungwa mkono na
mabadiliko ya kiulimwengu ya kisiasa hasa kuanguka kwa dola za
kisoshalisti(dola ya Ulaya Mashariki). Anguka hilo kulifanya jumuiya za
Ulaya Mashariki kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi na baadaye kusambaa
duniani kote”.
Nchini
Tanzania uanzishwaji wa mfumo wa vyama vingi vya siasa ulianza kwa
serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Tume ya kuratibu
maoni ya watanzania juu ya mfumo gani wa siasa utafatwa nchini. Tume
hiyo iliyoongozwa na Marehemu Jaji Nyalali ilikusanya na kuratibu maoni
ya wananchi katika sehemu mbali mbali.
Tume
hiyo ilipokamilisha kazi hiyo, ripoti ilionyesha maoni ya watanzania
wachache asilimia 20 ndio waliokubali mageuzi ya vyama vingi na asilimia
80 walipendelea Tanzania ibaki na mfumo wa chama kimoja.
Serikali ilianza kufuata maoni ya wachache ya kuanzisha mfumo wa vyama vingi. Hatua hiyo ilikua
ni uamuzi wa busara kwani ndani ya mfumo huu kuna ushindani wa fikra,
mawazo na hatimaye sera na taratibu mbadala za kuongoza nchi kwa misingi
madhubuti ya kidemokrasia yenye kuheshimu utu na kulinda haki za
binadamu.
Hali hiyo huleta msukumo katika harakati za kimaendeleo, ustawi wa maisha na kuzidisha umoja wa haki kwa watu.
Aidha
mfumo huo wa vyama vingi nchini ulionekana kama chuo cha siasa za
kiukombozi na upanuzi wa wigo wa demokrasia. Jambo hili linajidhihirisha
katika chaguzi mbali mbali ambapo wananchi wanapata nafasi ya kuchagua
viongozi wa kutoka vyama tofauti vya siasa , kuanzia madiwani, wajumbe
na wabunge.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini,
Tanzania kuna vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu 19, na chama
kimoja kina usajili wa muda.
Baadhi
ya vyama hivyo ni chama cha Mapinduzi (CCM), chama cha Wananhi (CUF),
chama cha demokrasia (CHADEMA), Tanzania Labour Party (TLP),
NCCR-Mageuzi, ACT Wazalendo na TADEA.
Vyama
hivi vya siasa vinafanya kazi chini ya Msajili wa vyama vya siasa
ambaye ni mwenye dhamana ya kuvisajili na kufuta ambavyo vinakiuka
kanuni za maadili ya vyama hivyo za mwaka 1992.
Akizungumzia
majukumu ya Ofisi yake Msajili wa vyama hivyo Mheshimiwa Jaji Francis
Mutungi alisema kuwa ni pamoja na kugawa ruzuku ya serikali kwa vyama
hivyo, kufatilia mapato na matumizi ya vyama hivyo na kusimamia
utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992na sheria
ya gharama za uchaguzi namba 6 ya mwaka 2010.
Vyama
vya siasa pia vina haki na wajibu unaoviongoza katika shughuli zake za
kisiasa. Haki hizo ni pamoja na kutoa elimu ya uraia na elimu ya
uchaguzi kwa wananchi kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi, kutoa
maoni ya kisiasa, kujadili na kushindanisha sera za vyama vyao na
kushiriki uchaguzi unaoendeshwa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.
Aidha
vyama hivyo vina wajibu wa kujieleza kwa wanachama wake ili kuongeza
uadilifu wa kisiasa ndani na nje ya chama na kulaani na kuepuka vitendo
vya vurugu.
Nao
baadhi ya wananchi waliohojiwa kuhusu uwepo wa vyama vingi nchini,
waliipongeza serikali kwa kuruhusu mfumo huo na kusema kwamba kwa sasa
wananchi wengi wanafahamu siasa za nchi pia uwepo wa uwakilishi wa
wabunge kutoka vyama mbali mbali bungeni kunaleta changamoto za
uwajibikaji zaidi na kuleta maendeleo kwa wananchi waliowachagua.
No comments:
Post a Comment