Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na waandishi wa habari
(hawapo pichani), kuhusu utekelezaji wa sheria ya EPOCA kulingana na
mabadiliko yaliyofanywa katika Sheria ya Fedha No. 2 ya mwaka 2016,
jijni Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa waandishi wa
habari (hawapo pichani), kuhusu umuhimu wa Kampuni za Mawasiliano
kujisajili katika Soko la Hisa kama Sheria inavyoelekeza, jijni Dar es
Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amezitaka Kampuni za Mawasiliano
kukamilisha taratibu za usajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam kwa
kuuza asilimia 25 ya hisa zote kadri ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na
Dhamana inavyoelekeza mwishoni mwa mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam,
Prof. Mbarawa ametaja kampuni hizo kuwa ni zile zenye leseni za
mawasiliano zilizotolewa kabla ya tarehe 1 Julai 2016 kwa ajili ya
Miundombinu ya Mawasiliano, Huduma za Mawasiliano, na Huduma za
Matumizi.
“Watoa huduma wote wa Mawasiliano
wajisajili na kuuza hisa zao kwa wananchi ndani ya mwezi wa Disemba”,
amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa kwa Kampuni
zilizopata leseni baada ya tarehe mosi Julai, 2016 watatakiwa kutimiza
sharti hilo la kisheria kwa kipindi kisichozidi miaka miwili tangu
kusajiliwa.
Waziri Prof. Mbarawa amesisitiza
kuwa Kampuni zitakazokiuka Sheria hiyo zitachukuliwa hatua za kisheria
kupitia kifungu cha 21 (C) cha EPOCA, 2010.
Aidha, amewataka wananchi kutumia
fursa hiyo kununua hisa hizo na kuwa sehemu ya wamiliki wa makampuni ya
Mawasiliano ili kuongeza kipato na kushiriki katika maamuzi ya kampuni
hizo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment