Wakati mwili wa Mwanahabari, Mpoki
Bukuku ukiagwa leo jijini Dar es Salaam, Rais wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Theophil Makunga kutokana na
kifo hicho.
Mpoki Bukuku alifariki dunia
Ijumaa iliyopita, alipokuwa akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili, Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya
kujeruhiwa vibaya kwa kugongwa na gari eneo la ITV Barabara ya Bagamoyo
jijini.
Hadi mauti yanamkuta akiwa na umri
wa miaka 44, Mpoki alikuwa Mpigapicha wa magazeti ya The Guardian
ambako kabla aliwahi kufanya kazi kwa mafanikio makubwa katika kampuni
za Mwananchi Communications na Business Times – zote za Dar es Salaam.
Rais Malinzi alipokea taarifa za
kifo cha mwanahabari huyo kwa masikitiko makubwa na katika salamu za
rambirambi pia zimekwenda kwa familia ya marehemu Mpoki Bukuku, ndugu,
jamaa na marafiki na kuwataka kuwa na moyo wa subira wakati huu mgumu wa
msiba wa mpendwa wao.
Rais Malinzi alimwelezea Mpoki
Bukuku, wakati wa uhai wake alikuwa na mchango mkubwa katika tasnia ya
habari za michezo akitoa mawazo yake hivyo ameacha alama ya ucheshi,
kujituma na uwajibikaji katika kufanikisha kazi zake katika vyombo vya
habari alivyofanyia kazi.
Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu Mpoki Bukuku mahala pema peponi.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment