Msimamizi
wa Mradi wa ujenzi wa Kituo cha kuzalisha Umeme cha Kinyerezi II,
Mhandisi Bernd Siegemund akitoa maelezo ya historia ya mradi huo kwa
maofisa wa ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Tume ya Mipango wakati
wataalam hao walipofanya ziara kukagua maendeleo ya ujezi wa kituo
hicho.
Msimamizi
wa Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha kuzalisha Umeme cha Kinyerezi II,
Mhandisi Bernd Siegemund akiweka bayana mipango na mikakati ya
kumalizika kwa ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi II
katika muda uliopangwa. Wengine ni wataalam kutoka Tume ya Mipango,
wataalam kutoka TANESCO pamoja na wahandisi wanaotekeleza mradi huo.
Mhandisi
Omari Athuman (aliyeshika notebook) kutoka Tume ya Mipango akitoa
ushauri kwa mkandarasi wa mradi wa ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme
cha kinyerezi II.
Picha
ya pamoja kati ya wataalamu kutoka Tume ya Mipango, wataalam kutoka
TANESCO pamoja na wahandisi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa kituo cha
kuzalisha umeme cha kinyerezi II.
Shughuli za ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme cha kinyerezi II zikiendelea.
Moja ya sehemu ziliyojengwa kwa ajili ya kusimika mitambo ya kuzalisha umeme.
Na Adili Mhina, Dar
Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya
Maendeleo kutoka Tume ya Mipango imetembelea mradi wa ujenzi wa kituo
cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi II kwa lengo la kuangalia maendeleo ya
kituo hicho ambacho kinatarajiwa kuzalisha kiasi cha megawati 240 pale
kitakapokamilika.
Akizungumzia juu ya maendeleo ya
mradi huo, msimamizi wa shughuli za ujenzi katika kituo hicho, Mhandisi
Bernd Siegemund kutoka Ujermani alieleza kuwa ujenzi wa kinyerezi II
unaendelea vizuri na unatarajia kukamilika kwa muda uliopangwa.
Ujenzi huo ulianza tarehe 13
Machi, 2015 na kutokana na kasi yake, Mhandisi Siegemund alieleza kuwa
matarajio ni kwamba hadi kufikia mwezi Novemba mwaka 2017 mtambo wa
kwanza utaanza kuzalisha umeme huku mitambo mingine ikiendelea kuwashwa
kadiri itakavyokuwa inakamilika.
Kuhusu vifaa vya ujenzi
vinavyohitajika, Mhandisi Siegemund alisema kuwa wanajitahidi kununulia
ndani ya nchi vifaa vyote vinavyopatikana na vinavyokidhi mahitaji
katika mradi huo na pale inapobidi hulazimika kuagiza kutoka nje.
Aliongeza kuwa pamoja na nondo
kuzalishwa ndani ya nchi wamelazimika kuagiza kutoka nje kwa kuwa
viwanda vya ndani bado havijazalisha aina ya nondo wanayohitaji katika
ujenzi wa kituo hicho.
“Vifaa kama saruji na vingine
tunaagiza kutoka kwa wazalishaji wa ndani ili kusaidia kukua kwa uchumi
wa nchi. Tulitaka kuagiza nondo hapa nchini lakini hatukupata kiwango
tunachohitaji kwa kuwa ujenzi huu hautumii nondo tulizozizoea katika
ujenzi wa kawaida,”alieleza Siegemund.
Aliongeza kuwa mradi huo
utakapokamilika utakabidhiwa na kuendeshwa na Shirika la Umeme nchini
(TANESCO) ambapo wataalam wa shirika hilo wanaendelea kupata elimu na
uzoefu katika kutumia mitambo ya kisasa zaidi na wanashirikishwa katika
kila hatua ya ujenzi wa kituo hicho.
Wataalam kutoka Tume ya Mipango
walipata fursa ya kukagua maeneo mbalimbali ya mradi huo ambao umesaidia
kupatikana kwa ajira takriban 400 katika ngazi mbalimbali na kumshauri
mkandarasi huyo kuendelea na kasi hiyo ili malengo ya Mpango wa Pili wa
Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21) pamoja na Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025 yafikiwe kwa haraka.
No comments:
Post a Comment