Waziri wa habari, utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye amesema amejifunza mengi kupitia kazi za mwandishi na mpiga picha wa kampuni ya TheGurdianLtd marehemu Mpoki Bukuku kutokana na mchango wake mkubwa katika tasnia ya habari.
"Bukuku ameacha pengo kubwa hivyo hatosahaulika.wanahabari hatuna cha kufanya ila tunamshukuru Mungu na kupitia kazi zake tujifunze yale yote aliyoyafanya," alisema.
Akisoma historia ya Bukuku, kaka wa marehemu, Alfred Mwakaposa alisema marehemu alizaliwa 15/3/1972 katika Hospitali ya Mount Meru mkoani Arusha, akiwa mtoto wa tano kwenye familia ya Bukuku.
Alisema alianza elimu ya msingi katika Shule ya Forodhani, Mlimwa Dodoma na baadae kuhamia Kisarawe, elimu ya sekondari alisoma Canon Andrea mkoani Dodoma na kidato cha tano na sita katika Shule ya Makumira Arusha.
"Baadaye marehemu alijiunga na elimu ya chuo cha uandishi wa habari TSJ ngazi ya cheti na Diploma. Amewahi kufanya kazi katika gazeti la Majira, Mwananchi na kuhamia Guardian mpaka mauti yalipomfika," alisema.
Akizungumza kwa niaba ya wasanii wa filamu, Muigizaji maarufu Steve Nyerere alisema tasnia ya filamu imepata pigo kubwa kumpoteza Bukuku hivyo wanaamini anapoenda ni sehemu nzuri.
"Nimemjua Mpoki wakati tupo Singida, tunaamini anapoenda Mpoki ni sehemu nzuri, tuko pamoja na familia yake, " alisema.
No comments:
Post a Comment