Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amewahimiza wakazi wa vijiji saba wilayani Ruangwa waharakishe kufyatua
matofali ili waanze ujenzi wa zahanati na yeye atawachangia mabati.
Ametoa ahadi hizo leo (Jumatano,
Desemba 28, 2016) wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Namilema,
Mbuyuni, Nandandara, Namkonjera, Muhuru, Chikundi na Chibula na
viongozi wa wilaya ya Ruangwa, mkoa wa Lindi ambako anapita kuwasalimia
wananchi wa jimbo lake na kuhimiza kazi za maendeleo. Waziri Mkuu yuko
Ruangwa kwa siku nne kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.
Amesema sera ya Serikali ni kuwa
na zahanati kwa kila kijiji na kituo cha afya kwa kila kata na kwamba
umefika wakati wa kuanza kutekeleza kaulimbiu ya jimbo hilo inayosema
“Ruangwa kwa maendeleo, inawezekana.”
Katika kuhimiza ujenzi wa zahanati
hizo, amechangia mabati kati ya 50 na 150 kwa kila kijiji na
akawahimiza wahakikishe wanakamilisha mapema ujenzi wa maboma ili aweze
kutimiza ahadi yake ya mabati.
Amesema katika awamu iliyopita,
alikazania sana suala la elimu kwa kusimamia ujenzi wa nyumba za walimu
na madarasa kwenye shule ambazo hazikuwa na madarasa ya kutosha. Pia
alisimamia ukarabati wa majengo chakavu katika baadhi ya shule.
“Kuanzia awamu hii na miaka minne
iliyobakia, mkakati wangu ni kusimamia upatikanaji wa maji safi na suala
la kuboresha sekta ya afya katika jimbo zima nikishirikiana na uongozi
wa Halmashauri yetu,” amesema.
Pia amemwagiza Mganga Mkuu wa
Wilaya hiyo, Dk. Japhet Simeo ahakikishe anawasiliana na viongozi wa
vijiji hivyo ili wapatiwe michoro ya ramani zilizoidhinishwa na Wizara
ya Afya.
Wakati huohuo, Mkurugenzi wa
kampuni ya Umemejua ya Baraka Solar Specialist, Bw. Ansi Mmasi amesema
atajitolea kuweka mfumo wa umemejua wa watts 300 pamoja na nyaya zake
kwenye zahanati inayotaka kujengwa kwenye kijiji cha Namilema.
Alisema anaishukuru kwa kuwapa
kazi makandarasi wazawa na akawataka wakandarasi wenzake watumie vifaa
bora na imara pindi wanapopewa kazi ya kutoa huduma na taasisi
mbalimbali ikiwemo halmashauri na idara za Serikali.
“Tujitahidi kufanya kazi hizi kwa
weledi na tutumie vifaa bora na imara ili watu wanaotarajia huduma zetu
waweze kuridhika na kuendelea kuwa na umani na wakandarasi wazawa kwamba
tunaweza kufanya kazi nzuri na zenye ubora unaotakiwa,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya
ujenzi ya Wanyumbani Construction, Bw. Fakihi J. Bakili alisema
atachangia mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo ya
kijiji cha Namilema. Pia alichangia mifuko 100 kwenye zahanati ya kijiji
cha Manokwe na mifuko mingine 50 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya
kijiji cha Chikundi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, DESEMBA 28, 2016.
No comments:
Post a Comment