Jeshi la Polisi mkoa wa
Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika
maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa
likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za
kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni
pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Katika kuelekea
sikukuu za mwisho wa Mwaka, Krismas na mwaka mpya 2017 Jeshi la Polisi
Mkoa wa Mbeya limejipanga vizuri kwa kuimarisha ulinzi na usalama katika
maeneo yote. Katika kuhakikisha wakazi wa Mkoa wa Mbeya wanasherehekea
kwa amani na utulivu sikukuu ya mwaka mpya, tumeandaa mpango mkakati
kama ifuatavyo:-
MPANGO MKAKATI WA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KUELEKEA SIKUKUU YA NA MWAKA MPYA:
- Ulinzi na usalama katika nyumba za ibada
Kwa makanisa ambayo yatakuwa na
ibada za mkesha kwa siku ya tarehe 31.12.2016 kutakuwa na askari ambao
wataimarisha ulinzi na usalama kwa kusaidiana na kamati ya ulinzi na
usalama ya kanisa/msikiti husika. Kuhakikisha ulinzi ndani na nje ya
kanisa/msikiti unakuwepo, ulinzi katika maeneo ya maegesho ya magari.
- Kumbi za starehe
Jeshi la Polisi linawataka
wamiliki wa kumbi za starehe kufuata na kuzingatia taratibu za
uendeshaji biashara zao hasa kwa kuzingatia muda wa kufungua na kufunga
kumbi zao kulingana na vibali vya biashara zao, kuzingatia idadi ya watu
wanaopaswa kuingia ukumbini kulingana na ukubwa wa ukumbi ili kuepuka
madhara yanayoweza kujitokeza. Pia tunawataka kuweka walinzi wa ndani ya
ukumbi na nje hasa maeneo ya maegesho ya magari ili kudhibiti uhalifu
na wahalifu.
- Waendesha vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara.
Kutokana na kuwepo ongezeko la
vyombo vya moto katika Mkoa wa Mbeya magari, pikipiki na bajaji kila
mtumiaji wa vyombo hivi anatakiwa kuzingatia utimilifu wa afya yake,
usalama wa chombo chake pamoja na kuheshimu, kufuata na kuzingatia
sheria na alama za usalama barabarani. Aidha watembea kwa miguu
kuhakikisha wanakuwa waangalifu wakati wa kuvuka barabara ili kuepuka
ajali. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga vizuri kuhakikisha
usalama kwa watumiaji wa vyombo vya moto na watumiaji wengine wa
barabara unakuwepo, pia kwa wageni wanaoingia na kupita kuelekea nchi
jirani na mikoa jirani wanapita bila usumbufu wowote.
- Uangalizi wa watoto katika kipindi chote cha sikukuu.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya
linawataka wazazi na walezi kuhakikisha kila mmoja anakuwa makini na
mtoto wake kwa kutoa uangalizi katika kipindi chote cha sikukuu ya mwaka
mpya. Kuhakikisha watoto wanakuwa na waangalizi pindi wanapotoka kwenda
maeneo ya mbali kama vile sehemu za kuabudu makanisani na misikitini,
sehemu za michezo ya watoto ili kuepuka matukio ya kupotea kwa watoto na
hata kuepuka vitendo vya uhalifu dhidi ya watoto. Aidha ni wito wa
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kila mzazi, mlezi na jamii kwa ujumla kuwa
makini na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pindi wanapoona
mtoto/watoto waliopotea.
- Ulinzi na usalama katika nyumba za kuishi/makazi yetu
Pia ulinzi na usalama ni muhimu
katika makazi yetu, vikundi vya ulinzi shirikishi vilivyopo katika mitaa
vina kazi ya kufanya katika kipindi hiki kutokana na ongezeko la watu.
Aidha Jeshi la Polisi litakuwa pamoja na vikundi hivi kufanya doria ya
pamoja katika maeneo tete na makazi. Pia ni rai yangu kwa kila mmoja
kuhakikisha anapotoka anaacha mtu/muangalizi ili kuepuka vitendo vya
uvamizi, uvunjaji.
WITO WA KAMANDA.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya
Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wakazi
wa Mkoa wa Mbeya kwa ujumla kuwa watulivu, kusherehekea kwa utulivu na
amani sikukuu ya mwaka mpya 2017. Aidha anatoa wito kwa wananchi kuacha
kuzurura ovyo na pia kushirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi
pamoja na kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu katika maeneo yao.
Imesainiwa na:
[DHAHIRI A. KIDAVASHARI – DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.
No comments:
Post a Comment