Saturday, 31 December 2016

Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa amewaasa Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza nchini kuzingatia kuwa utendaji wao wa kazi za kila siku

timi
Na Lucas Mboje, Dar es Saam
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa(pichani) amewaasa Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza  nchini kuzingatia  kuwa utendaji wao wa kazi za kila siku uende sambamba na kasi ya Serikali ya Awamu ya tano ili kuleta ufanisi unaotarajiwa.
KAIMU Kamishna Jenerali, Dkt. Malewa ameyasema hayo jana wakati wa Baraza la Kufunga Mwaka 2016 na kuukaribisha Mwaka 2017 lililowahusisha baadhi ya Maafisa na Askari kutoka Ofisi ya Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga, Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani pamoja na Magereza ya Mkoa wa D’Salaam.
Aidha, amewataka Maofisa na Askari wa Jeshi hilo kudumisha nidhamu wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kazi  ikiwemo kutekeleza mara moja Amri mbalimbali zinazotolewa na Viongozi wao wa Jeshi.
“Kila mmoja wenu atimize wajibu wake katika eneo lake la kazi kwa bidii, ari na moyo wa kujituma ili kuliwezesha Jeshi letu kupata ufanisi unaotarajiwa”. Alisisitiza Kaimu Jenerali Dkt. Malewa.
Wakati huo huo Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa  pia ametumia fursa hiyo kuelezea baadhi ya mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kwa Mwaka uliopita 2016 ambapo Jeshi la Magereza limeweza kupata jumla ya leseni 102 za uchimbaji wa madini ya ujenzi kama vile chokaa, mawe, kokoto, mchanga na Murram katika maeneo mbalimbali ya magereza. Pia katika mwaka 2016 Jeshi limeweza kujenga nyumba 129 kwa njia ya kujitolea ambapo nyumba 231 zipo katika hatua mbalimbali ya ukamilishaji.

Aidha, Ujenzi wa nyumba 320 za makazi ya askari katika eneo la Gereza Ukonga maandalizi ya ujenzi yanaendelea na ujenzi wa nyumba hizo ni kufuatia ziara ya Rais Magufuli  Novemba 29 mwaka huu  ambapo alipokea taarifa ya uhaba wa nyumba za kuishi askari wa jeshi hilo na akaagiza Jeshi la Magereza lipatiwe Tsh. bilioni 10 haraka ili kupunguza tatizo hilo.
Shirika la Magereza na Mfuko wa hifadhi ya Jamii wa PPF wameingia Makubaliano ya Mkataba wa ubia katika mradi wa ujenzi wa Kiwanda kipya cha kusakata ngozi pamoja na uwekezaji wa mashine za kisasa za kutengnezea bidhaa za ngozi katika Kiwanda cha Viatu cha Gereza Karanga, Moshi.
Chuo cha Maafisa Magereza Ukonga kimepata Ithibati na hivyo kuwa na hadhi ya kuwa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji na mapema mwakani kinatarajia kudahili wanafunzi 30 katika fani ya Taaluma ya Urekebishaji ngazi ya cheti. 
Pamoja na Mafanikio hayo, Kaimu Kamishna Jenerali Dkt. Malewa ameelezea changamoto mbalimbali zinazolikabili Jeshi hilo ikiwemo ufinyu wa bajeti, makazi duni ya maofisa na askari, uhaba wa vitendea kazi, ukosefu wa pembejeo pamoja na madeni ya wabuni na watumishi wa jeshi hilo.

Kuhusu maeneo yatakayopewa kipaumbele kwa Mwaka mpya 2017 ni kuwa Jeshi la Magereza litaendeleza jitihada za kuimarisha na kuongeza uzalishaji kwenye miradi ya uzalishaji wa mazao ya Kilimo na mifugo lengo ikiwa ni kujitosheleza kwenye chakula cha wafungwa, kuhakikisha wafungwa wanafanya kazi za uzalishaji mali kwa kiwango chenye tija badala ya kukaa tu magerezani pia kuendeleza mikakati ya kupunguza msongamano magerezani.
Baraza la kufunga Mwaka na kuukaribisha Mwaka unaofuata ni utamaduni wa siku nyingi ambao unaenziwa na Viongozi Wakuu wa Jeshi la Magereza ambapo Baraza la aina hii hufanyika kila Mwaka ili Kamishna Jenerali wa Magereza nchini aweze kuongea na Watumishi wote wa Jeshi la Magereza nchini kupitia Baraza hilo lengo ikiwa ni kufanya tathmini ya yale yaliyojiri katika Jeshi kwa kipindi cha Mwaka unaisha kwa kuzungumzia mafanikio na changamoto zilizojitokeza na  kutazama matarajio ya Mwaka mpya.

No comments:

Post a Comment