Ndugu Watanzania, Kama mnavyofahamu kuwa
ibara ya 132(4) na (5) na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheria
namba 13 ya mwaka 1995 inataka viongozi wote wa umma kujaza fomu za
Tamko la Rasilimali na Madeni. Tamko hilo huwasilishwa Sekretariat ya
Maadili ya Viongozi kabla ya mwisho wa kila mwaka. Kama nifanyavyo siku
zote, nawajulisha rasmi kwamba nimetimiza matakwa hayo ya katiba na
sheria kuhusu Maadili ya Viongozi.
Inafahamika kuwa Chama Cha ACT Wazalendo,
kwa mujibu wa Katiba yake na Azimio la Tabora, kimeelekeza kuwa Viongozi
wake wote waweke wazi kwa Umma Tamko la Mali, Madeni na Maslahi. Kwa
kufuata masharti ya Katiba ya Chama Cha ACT Wazalendo natangaza rasmi
fomu zangu nilizowasilisha Leo Sekretariat ya Maadili ya Viongozi wa
Umma.
Ni matumaini yangu kwamba itafikia wakati
Daftari la Rasilimali na Madeni la Viongozi wa Umma litakuwa linawekwa
wazi kwa Umma ili wananchi waweze kujua Mali, Madeni na Maslahi ya
Viongozi wao na pale ambapo kiongozi ametoa habari zisizo sahihi au
kuficha mwananchi aweze kutoa Taarifa kwenye Sekretariat na Baraza la
Maadili liweze kufanya kazi yake ipsavyo.
Mfumo wa kuweka wazi Rasilimali na Madeni
ya Viongozi wa Umma ni mfumo endelevu na muhimu kwenye vita vita dhidi
ya ubadhirifu na ufisadi. Mataifa kadhaa duniani hutumia mfumo huu (
public disclosure of leaders’ assets and liabilities) kuwezesha
mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Nchini Uingereza na Kanada kwa
mfano, daftari la matamko ya Rasilimali na Madeni ya Viongozi lipo wazi
kwa kila mwananchi kuona na huuzwa kwenye duka la vitabu la Bunge.
Namsihi Sana Rais John Pombe Magufuli
kusaidia kufanya mabadiliko makubwa ya Sheria ya maadili ya Viongozi ili
kurejesha na kuboresha Miiko ya Viongozi katika kuimarisha vita dhidi
ya ufisadi nchini. Rais aliahidi kuweka wazi Mshahara wake alipokuwa
anazungumza katika kipindi cha 360 cha Clouds TV. Ninamkumbusha afanye
hivyo na pia aweke wazi Mali, Madeni na Maslahi yake ya Kibiashara ili
awe mfano kwa Viongozi wengine Nchini.
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
Kigoma Mjini
30/12/2016
No comments:
Post a Comment