Nahodha wa Klabu Bingwa ya Afrika
Mashariki na Kati Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, amewatakia mashabiki
wa timu hiyo kheri ya mwaka mpya ‘2017’ unaoanza leo saa 6.00 usiku huu
huku akiwashukuru kwa sapoti yao waliyoionyesha mwaka huu.
Bocco ametoa kauli hivi karibuni
mara baada ya kumalizika kwa mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania (VPL) dhidi ya Tanzania Prisons walioifunga bao 1-0, huku
akifanikiwa kutupia bao hilo pekee lililorudisha morali ndani kikosi
hicho baada ya kutofanya vizuri kwenye mechi mbili za ufunguzi wa
mzunguko wa pili walipocheza ugenini na African Lyon (0-0) na Majimaji
(1-1).
“Kwanza tunawashukuru mashabiki
wetu kwa uvumilivu waliouonyesha, kwa sapoti waliotupa katika kipindi
chote kigumu tulichopitia, kama wachezaji na timu kwa ujumla tunawaomba
waendelee kuwa na moyo huo huo na pia tunawatakia kheri ya mwaka mpya
(2017) na wamalize mwaka huu vizuri, tuendelee kuwa pamoja ili kuisaidia
timu yetu iweze kufanya vizuri,” alisema Bocco wakati akizungumza na
mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz
Bocco ambaye ameipatia mafanikio
makubwa Azam FC kwa mabao yake muhimu tokea timu hiyo ikiwa madaraja ya
chini hadi kupanda Ligi Kuu mwaka 2008, aliendelea kusema kuwa wamepitia
changamoto nyingi sana kwa mwaka huu unaoisha huku akidai kuwa
wamejifunza kupitia hayo na wanachoangalia kwa mwaka mpya ni kuipeleka
mbele zaidi timu hiyo ili kufikia mafanikio.
“Changamoto zilikuwepo nyingi na
ni sehemu ya maisha, sisi kama timu tunajua mpira unachangamoto zake na
tumezipokea kama binadamu na sisi wachezaji changamoto iliyokuwa katika
kazi yetu haikuwa ndogo na tunamshukuru Mungu kwa kuweza kutusaidia
tumeweza kupigana nazo na hatukuweza kukata tamaa, kikubwa tunachofanya
hivi sasa ni kuangalia mbele zaidi ili kuipatia timu mafanikio kwa mwaka
unaokuja,” alisema.
Azam FC mbali na kuwa bingwa
mtetezi wa michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA
Kagame Cup), inamaliza mwaka huu ikiwa imefanikiwa kukata tiketi ya
kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani pamoja na taji
la Ngao ya Jamii baada ya kuichapa Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-1
kufuatia sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90 za mchezo huo uliofungua
pazia la ligi msimu huu.
Ujio wa Mapinduzi Cup
Wakati kikosi cha timu hiyo
kikielekea mchana wa leo Jumamosi visiwani Zanzibar kwenda kushiriki
michuano ya Kombe la Mapinduzi, Bocco amesema kuwa wao kama wachezaji
wanaenda kushindana na hatimaye kurejea na ubingwa wa michuano hiyo.
“Mashindano ya Mapinduzi si mageni
kwa Azam FC, michuano hiyo si mepesi ni migumu, sisi kama wachezaji
tunaenda kushindana naamini ni sehemu moja ya msimu huu ambayo tukiweza
kuchukua kombe itakuwa ni faraja kwa klabu na mashabiki wetu pamoja na
sisi wachezaji, tukitoka huko hata tukirudi kwenye ligi tutakuwa na
morali nzuri ya kuendeleza ushindi kwenye ligi, michuano ya FA na Kombe
la Shirikisho Afrika,” alimalizia Bocco.
Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji
safi cha Azam Cola kinachosisimua mwili na kuburudisha koo pamoja na
Benki ya NMB, inaenda huko ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kulitwaa taji
hilo mara mbili (2012,2013), ambapo itaanza kufungua dimba Jumatatu
ijayo kwa kuvaana na Zimamoto saa 10.15 jioni.
Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii wapo Kundi B pamoja na timu nyingine za Yanga na Jamhuri.
No comments:
Post a Comment