






Wasanii wakubwa nchini kulishambulia
jukwaa, wakiwemo Ali Kiba, Lady Jaydee, Yamoto Band, Madee, Juma Nature,
Snura, Stamina, Eskide (msanii wa muziki wa singeli) na bila ya kusahau
wakali wa bongo movie pia watakuwepo.
Wasanii wa muziki wa Bongo Flava
Ali Kiba na Lady Jaydee wanatarajiwa kutumbuiza katika tamasha la
kusherehekea miaka miwili tangu kuanzishwa kwa chaneli ya StarTimes
Kiswahili siku ya Jumamosi ya Agosti 13, 2016 katika viwanja vya Posta,
Kijitonyama.
Akizungumza na waandishi wa
habari kuhusiana na tamasha hilo Mkurugenzi Msaidizi wa Masoko na
Maudhui wa StarTimes Tanzania, Bw. Damien Li amesema kuwa tamasha hilo
linadhamiria kusherehekea kwa pamoja na wateja wao mafanikio
yaliyofikiwa na chaneli ya StarTimes Kiswahili katika kuonyesha vipindi
vyenye maudhui ya Kiswahili nchini Tanzania na Kenya.
“Chaneli hii mwaka huu mwezi wa
Agosti inatimiza miaka miwili tangu kuanzishwa kwake mnamo Agosti mosi
mwaka 2014. Chaneli ya StarTimes Kiswahili inaonekana katika nchi mbili
za Tanzania na Kenya na hivyo kutoa wigo mpana kwa wasanii na
watayarishaji wa vipindi hapa nchini kupata fursa ya kuonekana maeneo
hayo. Vipindi vingi katika chaneli hii huangazia masuala ya filamu,
muziki, burudani, vyakula, mitindo ya maisha na mavazi pamoja na
tamaduni za watu wa Afrika ya Mashariki hususani kwa nchi hizo mbili
ambavyo huwasilishwa kwa lugha ya Kiswahili.” Alisema Bw. Li
“Tamasha hili litahusisha
shughuli mbalimbali hususani kuangazia maudhui yanayopatikana kwenye
chaneli ya StarTimes Kiswahili lakini pia litapambwa na burudani kadhaa
kutoka kwa wasanii watakaoalikwa. Siku hiyo watanzania watawashuhudia
wasanii wakubwa wa muziki wa bongo flava jukwaani kama vile Ali Kiba,
Lady Jaydee, Juma Nature, Madee, Yamoto Band, Snura na Stamina. Pia
kutakuwepo na wasanii mashuhuri kutoka katika tasnia ya bongo movie
ambao filamu zao zinaonekana kupitia chaneli hii kama vile Wema Sepetu,
JB, Steve Nyerere na Ray Kigosi.” Aliongezea Bw. Li
Chaneli ya StarTimes Kiswahili
inapatikana katika visimbuzi vyote viwili vya StarTimes yaani cha
antenna kuazia kifurushi cha NYOTA kwa shilingi 6000/- na cha dishi
kuanzia kifurushi cha NYOTA PLUS kwa shilingi 8000/- kama malipo ya
mwezi. Kampuni hiyo inajivunia kuwa ya kipekee nchini Tanzania kwa kutoa
matangazo bora ya dijitali kwa gharama nafuu ambayo kila mtu anaweza
kuimudu.
“Ningependa kutoa wito kwa wateja
wa StarTimes na watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika
tamasha hili litakalofanyika siku ya Jumamosi ya Agosti 13 mwaka huu
pale viwanja vya Posta, Kijitonyama jijini Dar es Salaam. Tiketi
zitapatikana kwa bei ya kawaida kabisa ya kuanzia shilingi 5000/- na
kupatikana katika vituo vitakavyoanza kutangazwa kwa njia mbalimbali.
Tamasha hili ni maalumu kwa ajili ya kuwashukuru watanzania kwa kuipokea
vizuri chaneli hii na kuifanya kuwa chaguo lao kubwa pindi watazamapo
luninga, hivyo naomba wajitokeze kwa wingi.” Alimalizia Bw. Li
Naye kwa upande wake msanii wa
bongo flava Ali Kiba akizungumza mbele ya waandishi wa habari amewaahidi
makubwa wateja wa StarTimes na watanzania watakaohudhuria siku hiyo
kuwa watapata burudani ya aina yake.
“Kwanza kabisa ningependa kutoa
pongezi za dhati kwa kampuni ya StarTimes kwa kutambua mchango wa lugha
ya Kiswahili na kuikuza miongoni mwa nchi wanazofanya biashara. Hii ni
fursa ya kipekee kwa wasanii na watayarishaji wa kitanzania kuweza
kupanua wigo wa kazi zao na kuweza kuonekana sehemu zingine. Kusema
ukweli hapo awali wakati matangazo ya dijitali yanaingia nchini sikuweza
kuiona fursa hii lakini sasa ninaona kazi za wasanii wetu zinaonekana
na kutambulika kimataifa.” Alisema Ali Kiba
“Ningependa kutoa wito kwa
StarTimes kupanua wigo zaidi wa chaneli hii ifike katika nchi zingine za
jirani kama vile Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Kongo hata Afrika ya
Kusini kwani kuna watanzania kule na waafrika ambao wanapenda kufahamu
lugha ya Kiswahili na tamaduni za waswahili wenyewe. Na mwisho kabisa
ningependa kuwaalika watanzania wote siku hiyo waweze kuhudhuria kwa
wingi kwani tamasha hili ni lao, nawaomba waje kwa wingi kusherehekea
kwa pamoja maudhui mazuri na ya kusisimua yanayopatikana ndani yake.”
Alihitimisha Ali Kiba au King Kiba kama anavyojulikana miongoni mwa
mashabiki wake
No comments:
Post a Comment