Wednesday, 4 October 2017

Umoja wa Mataifa wamevionya vyama vya siasa vya Jubilee na muungano wa upinzani (Nasa}

  Image result for uhuru kenyatta na odinga
 Kenya. Umoja wa Mataifa umevionya vyama vya siasa vya Jubilee na muungano wa upinzani (Nasa) dhidi ya kusudio la kususia uchaguzi wa marudio kwa kura ya urais Oktoba 26 kwamba linaweza kuitumbukiza nchi katika mgogoro.
Lakini pia Umoja wa Mataifa umevipongeza vyama vyote kwa kushiriki kikao kilichoitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) kujadili maandalizi ya uchaguzi huo wa marudio.
Katika taarifa yao ya Jumatano, Umoja wa Mataifa umezitaka pande mbili hizo kuhakikisha nchi inabaki na umoja baada ya uchaguzi. "Wajibu wa kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa mafanikio siyo tu kwamba uko katika mikono ya tume ya uchaguzi bali pia ushiriki mpana wa wadau wote," imesema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Nasser Ega-Musa, Mkurugenzi wa UN katika kituo cha habari.
Umoja huo umesema vyama vya siasa, wafuasi wao, asasi za kijamii na wapigakura wote kwa ujumla wao wanapaswa kuhakikisha uchaguzi unafanikiwa.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amedokeza uwezekano wa kususia uchaguzi huo endapo matakwa waliyowasilisha IEBC hayatazingatiwa.
Soma: Mbunge ataka mahakama imzuie Raila kususia uchaguzi
Jumanne, viongozi wa Nasa walisema inasikitisha kwamba IEBC inawapatia ripoti ya nini wanafanya na siyo nini wanapaswa kufanya kurekebisha makosa yaliyochangia matokeo ya kura ya urais kwa uchaguzi wa Agosti 8 kufutwa.
Seneta wa Siaya James Orengo alisema hakuna "sharti hata moja” lililotekelezwa na IEBC.
Miongoni mwa masharti ambayo Nasa wanataka yatekelezwe kwanza ndipo washiriki uchaguzi ni kuondolewa maofisa 12 wa IEBC akiwemo mtendaji mkuu Ezra Chiloba pamoja na kuondolewa kampuni ya OT-Morpho iliyosambaza vifaa vya utambuzi wa mpigakura (KIEMS) na kampuni ya uchapaji kura ya Al-Ghurair.
Lakini Jubilee wamesema hawana masharti yoyote. Katika kikao cha jana Odinga aliongoza msafara wa Nasa kwenda IEBC lakini Rais Uhuru Kenyatta alimtuma makamu wake William Ruto.


Tume katika taarifa yake wiki iliyopita ilisema inataka kukutana na wagombea urais wenyewe na siyo wawakilishi. Tume imepanga kikao kingine baadaye.

"Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa wadau wote kuheshimu uhuru wa kikatiba ambao taasisi zimepewa hasusan IEBC na Mahakama."

No comments:

Post a Comment