NA VICTOR MASANGU, PWANI
KATIKA kukabiliana na kupambana
na wimbi la wizi linalofanywa na baadhi ya wamiliki wa magari na
pikipiki kuamua kutumia stika za bima bandia hatimaye Mamlaka ya
Usimamizi wa shughuli za bima nchini (TIRA) imeamua kutoa mafunzo kwa
askari wa kikosi cha usalamaa barabarani Mkoa wa Pwani kwa lengo la
kuwapa uelewa.
Akizungumza katika mafunzo hayo
ambayo yamewashilikisha maafisa wa polisi pamoja na askari wa kikosi cha
usalama barabarani Kamishina mkuu wa (TIRA) nchini Baghayo Sakwele
amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kwa ajili ya kuwafundisha askari
wa usalama barabarani mfumo mpya ambao utaweza kuwasaidia kutambua na
kuhakiki stika za bima ambazo ni bandia na zinatumika kinyume kabisa na
sheria na taratibu.
Kamishina huyo alibainisha kuwa
kwa sasa wameamua kushirikiana na jeshi la Polisi ili kufanya msako wa
kuwabaini wamiliki wa vyombo vya moto kutumia bima feki kitu ambacho
kinachangia kwa kiasi kikubwa kupotea kwa pato la Taifa kutokana na
vitendo vya wizi ambavyo vinafanyika, Ameongeza kuwa changamoto iliyopo
ni wamiliki wengine wanafanya ujanja wa kutumia bima moja zaidi ya
magari matano.
“Sisi kama TIRA ambao ndio wenye
mamlaka ya utoaji wa stika za bima katika vyombo vya magari, tumeamua
kushirikiana bega kwa bega na jeshi la polisi Mkoa wa Pwani ili
kuhakikisha kuwa baaadhi ya wamiliki waliokuwa na tabia ya kutumia
magari yao au pikipiki kwa kutumia bima bandia tunawakamata na
kuwachukulia hatua kali za kisheria na katika hili hatuwezi
kuwavulimilia hata kidogo,”alisema Kamishina Sakwele.
Kwa upande wake Kaimu kamanda wa
jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani Blasilusi Chatanda alisema kuwa
atalivalia njuga suala hilo la kufanya msako mkali ili kubaini mtandao
unaojihusiha na kutengeneza bima feki ili kuwadhibiti wale wote ambao
walikuwa wanatumia bima bandia kuwachukulia hatua kali za kisheria ili
iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
“Kama jeshi la Polisi Mkoa wa
Pwani kwa kushirikiana na wenzetu wa Tira kwa kweli tutashirikiana nao
kwa hali na mali na kwa kuwa wameshatupatia mafunzo kuhusiana na mambo
mbali mbali ikiwemo kuwepo kwa wimbi la madereva na wamiliki wa vyombo
vya moto kuwa na tabia ya kutumia stika za bima feki tunawakamata na
kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa hivyo askari wetu nina imani
walilifanikisha suala hilo,”alisema Kamanda.
Nao baadhi ya askari wa kikosi
cha usalama barabarani Mkoa wa Pwani ambao wameshiriki katika mafunzo
hayo akiwemo George Peter, Laitiness Kimaro pamoja na Khalid Mohamed
wamesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia katika kutekeleza majukumu yao
ipasavyo katika masuala mbali mbali ya kuwaelimisha madereva wa magari
na pikipiki kuhusiana na bima bandia na iliyo halali.
Walisema kuwa wana imani kuwa
baada ya kujifunza mafunzo hayo wataweza kufanya kazi zao za barabarani
kwa ufanisi mkubwa zaidi na kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa
madereva wote wa vyombo vya moto ikiwemo magari pamoja na pikipiki
kuhusiana na matumizi halali ya ukataji wa bima zao pamoja na madhara ya
kukata bima amabazo ni feki.
“Kwa kweli sisi kama askari wa
kikosi cha usalama barabarani katika Mkoa wa Pwani tumefarijika sana
kuaptiwa mafunzo haya na wenzetu wa mamlaka ya husika, hivyo na sisi
tutahakikisha elimu hii inakuwa ni chachu na mkombozi mkubwa katika
utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku pindi tunapokuwa barabarani
hivyo ni jambo ambalo kwa kweli ni faida kwetu,”walisema askari hao.
ASKARI hao wa kikosi cha usalama
barabarani Mkoa wa Pwani mara baada ya kupatiwa mafunzo hayo walikwenda
kufanya ukaguzi wa magari barabarani kwa njia ya vitendo zaidi ambapo
katika zoezi hilo wamefanikiwa kukamata baadhi ya magari na kuyapiga
faini ambayo yamekuwa bado yakiendelea kutumia bima feki kinyume na
sheria za nchi.
No comments:
Post a Comment